Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, imemhukumu kifungo cha maisha jela Maduhu Tarasisi Chubwa mwenye umri wa miaka 60 mkazi wa Nyihogo katika Manispaa ya Kahama, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka miwili.
Kesi hiyo ilikua inaendeshwa chini ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kahama Christine Chovenye ambapo Maduhu alidaiwa kutenda kosa hilo Novemba 11, 2020 katika kata ya Nyihogo, Manispaa ya Kahama majira ya saa nne mchana.
Hakimu iliiambia mahakama kuwa baada ya kujiridhisha na mashahidi walioshuhudia kitendo hicho kutoka eneo la chumba cha jirani, ushahidi mwingine uliomtia hatiani mwanaume huyo ni mbegu za kiume zilizokutwa katika sehemu za siri za mtoto huyo.
Daktari Idd Ramadhani kutoka hospitali ya Manispaa ya Kahama aliileza Mahakama kwamba baada ya kumkagua binti huyo alimkuta akiwa na mbegu za kiume pamoja na michubuko katika sehemu zake za siri.
Mtuhumiwa alipewa nafasi ya kujitetea baada ya hukumu, ambapo alisema anaomba apunguziwe adhabu kwani yeye ni Mzee wa miaka 60. Mahakama ilitupilia mbali utetezi huo.