Ifahamu historia ya Haji Manara

HomeMichezo

Ifahamu historia ya Haji Manara

Miaka ya 1970, Tanzania ilimshuhudia Sunday Manara, mzaliwa wa Kigoma aliyejaaliwa ufundi wa kusakata kabumbu. Sunday alifahamika kama ‘computer’ kutokana na ufundi wake wa kipekee uwanjani.

Januari 18, 1976, Sunday Manara alijaaliwa mtoto wa kiume, akamuita Haji, ndiye huyu ambaye leo jina lake linasikika sana, akiitwa ‘Bugati’.

Elimu

Haji Manara alianza masomo ya elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja kisha akaenda kuhitimu katika Shule ya Msingi Bunge (zote za Dar es Salaam). Kidato cha kwanza hadi cha nne alisoma katika Shule ya Sekondari Chimala, kisha kidato cha tano na sita alisoma katika Shule ya Sekondari Mzumbe mkoani Morogoro.

Baba yake alimpeleka Saudi Arabia kupata mafunzo ya dini, kabla ya kwenda Afrika ya Kusini alikosomea mawasiliano ya umma (Mass Communications).

Kazi

Baada ya kutoka Afrika Kusini, Haji alifanya kazi katika kituo cha Redio Uhuru ambapo alikuwa anatangaza vipindi vya michezo na siasa. Kisha aliajiriwa na kampuni ya Index International.

Mwaka 2007, aliteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kujiuzulu mwaka 2010 kufuatia shutuma nzito za utapeli na wizi wa magari. Haji alipelekwa mahakamani na baadaye mahakama ilimkuta hana hatia.

Mwaka 2015 Haji Manara alijiunga na timu ya Simba kama Afisa Habari (Msemaji) kazi ambayo aliifanya hadi Agosti 2021 ilipotangazwa kwamba ameondoka Simba.

Kwa sasa Haji Manara yuko Yanga katika kitengo cha Habari na Mawasiliano, huku akizungumzwa sana kwa kuhamia katika timu ambayo amekuwa akiisimanga kwa miaka mingi.

Mapenzi ya Soka

Mpira ndio kitu anachokipenda zaidi Haji Manara, alikuwa mchezaji mzuri wa Kariakoo United na timu nyingine alizochezea akiwa mwanafunzi. Tangu akiwa mdogo anafahamika kuwa shabiki wa timu ya Simba, licha ya kwamba baba yake na familia yote ni wapenzi wa Yanga. Inaelezwa kwamba Haji aliipenda Simba kupitia babu yake mzaa mama, marehemu Hassan Haji ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba.

Anachokifanya sasa ni kuunganisha kitu anachokipenda zaidi (mpira) na kile alichokisomea (habari na mawasiliano).

error: Content is protected !!