Manara ampiga kijembe Mo, Morrison aingilia kati

HomeMichezo

Manara ampiga kijembe Mo, Morrison aingilia kati

Tangu aliyekuwa Msemaji wa Simba SC, Haji Manara alipoondoka katika klabu hiyo kumekuwa na mfululizo wa matukio mbalimbali ambayo yalipamba moto zaidi alipojiunga Yanga SC.

Matukio hayo yamechagizwa na mambo ambayo Manara amekuwa akiyasema kuhusu waajiri wake hao wa zamani, ambapo amekuwa akisema ama kupitia vyombo vya habari au mitandao ya kijamii.

Leo ni siku nyingine na mvutano huo umehamia kwenye mtandao wa Instagram ambapo Manara ameandika ujumbe ambao aliyekuwa mchezaji wa Yanga ambaye sasa yupo Simba, Bernard Morisson amemjibu baada ya kuoneka kutofurahia kilichoandikwa.

Katika tafsiri isiyo ya moja kwa moja Manara amempiga vijembe aliyekuwa bosi wake, Mo Dewji (yeye hajamtaja) kwa njia ya kutoa sifa za bosi wa Yanga, GSM ambazo zinakinzana na za Dewji, akisisitiza kuwa mtu tajiri hapendi mbwembwe.

Manara ameandika “Lingine niwafahamishe Mukulu hatumii instagram,,, ukiona account yenye jina lake ni feki,,,, Matajiri huwa hawausiki na mitandao mara kwa mara, ? Wanatuachia cc [sisi] WAOMBA MUNGU,” ameandika Manara ikiwa ni wazi akimlenga Mo Dewji namna anavyotumia mitandao ya kijamii dhidi ya GSM ambaye hatumii.

Maneno hayo yamemwibua Morisson ambaye amesihi Manara kutomsema vibaya mtu au watu ambao wamewahi kumsaidia sehemu alikotoka. Morisson amesema aliondoka Yanga akiwa na mgogoro nao ambao bado upo lakini hajawahi kusema lolote baya kuhusu klabu hiyo.

“… unajua kwanini? ni kwa sababu walinilisha walinipenda na walinitendea vizuri mara nyingi sana hivyo siwezi kuwakosea heshima kwa sababu nina tatizo dhidi yao. Hiyo ni heshima na akili ya kawaida,” ameandika Morrison (tafsiri ya mwandishi).

Morrison ameenda mbali zaidi na kumtaka Manara kutong’ata mkono ambao umempa chakula.

Yanga na Simba zinavutana kuhusu usajili wa Morisson ambapo Yanga inadai kuwa wakati mchezaji huyo anasajiliwa alikuwa bado na mkataba na Yanga, wakati Simba ikidai alikuwa mchezaji huru. Uamuzi wa kesi hiyo ambayo ipo katika Mahakama ya Usuluhishi wa Kimichezo (CAS) utatolewa Septemba 21, 2021.

error: Content is protected !!