Watu wengi wanapenda sana watoto zao, na huonesha mapenzi hayo mara nyingine kwa kuwanunulia zawadi mbalimbali. Lakin wazazi wengi wamezoea viatu na nguo ndio zawadi kubwa inayofaa kumpa mtoto kama zawadi wakati wa msimu kama huu wa Sikukuu. Ukweli ni kwamba zipo zawadi nyingi na nzuri wazazi wasizofahamu ambazo wanaweza kuwapatia watoto wao, hasa wakati wa msimu kama huu wa sikukuu
Umepanga kumpa zawadi ipi mtoto wako? Hizi ni baadhi ya zawadi unazoweza kumpatia mtoto wako ili kumuongezea morali ya kusoma na hata kumjenga kiuchumi:
1.Simu janja, kompyuta ya kusomea.
Kwa wazazi walio karibu na watoto wao, wanafahamu mambo ambayo simu zao zinapitia punde tu wanapofika nyumbani. Watoto hupenda kutazama katuni, kucheza michezo na kufanya mambo mbalimbali kwenye simu za wazazi au ndugu na jamaa waliopo nyumbani.Katika msimu huu wa sikukuu, unaweza kuchagua kumnunulia mtoto wako tableti maalumu kwa ajili ya kujifunzia ikiwemo kuangalizia katuni na hata kucheza michezo.Unaweza kuzipata kwa bei kuanzia Sh150,000 katika maduka mbalimbali na gharama zinazoendana na uwezo wa uhifadhi.
2. Safari ya ndoto yake
Watoto hujifunza mambo mengi shuleni, mfano hujifunza nyimbo mbalimbali za mbuga za wanyama za ambazo wengine huishia kuziona kwenye picha au kusoma majina yake kwenye vitabu. Badala ya viwalo, mwaka huu unaweza kuchagua kumpeleka mtoto wako sehemu ya tofauti kama kwenye mbuga ambapo tunaamini, mtoto wako atapenda zaid. Wapo ambao kiu yao ni kwenda Kigamboni kuvuka bahari kwa pantoni na wengine shida yao ni kufika sehemu za chakula tu. Unaweza kuweka bajeti yako na kumpeleka sehemu ambapo mtoto wako ataweka tiki kwenye orodha ya sehemu za ndoto zake.
3. Vifaa vya kukuza talanta
Baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakichukulia poa talanta za watoto wao, wataalamu wa malezi wanashauri kwamba ni vyema ukamsoma mtoto na kumjua ni nini anataka na kupenda kufanya.