Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni, mkazi mmoja wa mkoani Mbeya, Saili Juma (27), amejikuta wilayani Masasi, mkoani Mtwara akiwa amelala juu ya mti fofofo Mtaa wa Misufini, Kata ya Migongo jambo liliostaajabisha na kuacha gumzo kwa wananchi wilayani Masasi huku likihusishwa na imani za kishirikina.
Juma alisema hafahamu amefikaje wilayani Masasi ilhali alikuwa nyumbani kwao Mbeya akiwa na bibi yake ambaye anaishi naye zaidi ya kwamba juzi usiku akiwa kwao alifanya shughuli zake za kila siku kama kawaida akiwa Mbeya na muda wa kulala aliingia chumbani kwake, lakini anashangaakujikuta Masasi bila kujitambua juu ya mti amelalla fofofo.
“Mimi ni mkazi wa Mbeya ndiko nyumbani kwetu na ninaishi na bibi yangu na mpaka jana usiku nimerudi kazini kwangu ninakouza CD za filamu na muziki na tumekula chakula pamoja na bibi, ila nashangaa saa hizi kujiona niko hapa wilayani Masasi nimefikaje ni swali ambalo hata mimi mwenyewe najiuliza,” alisema Juma kwa mshangao.
Akithibitisha tukio hilo Kaimu Kamanda wa Jesgi la Zimamoto na Uokoaji, Wilaya ya Masasi, Bakari Nirabu, alisema walipomshusha chini alikuwa hajitambui licha ya kumwagia maji baridi kama kumpatia huduma ya kwanza, hata hivyo hakuweza kuzinduka.
“Tulipigiwa simu na Jeshi la Polisi kuhusu kijana huyo na tulifika sehemu ya tukio tulimkuta kijana huyi akiwa amelala juu ya mti, tulimshusha chini na baadaye tulimkimbiza Hospitali ya Mkomaindo, lakini leo (juzi) asubuhi tumeshangaa tulioambiwa na wahudumu wa hospitali hiyo kuwa kijana huyo ni mkazi wa Songwe na hajui amefikaje wilayani Masasi,” alisema Kamanda Nirabu.