Reginald Mhango, aliingia Tanganyika mwanzoni mwa miaka 60 akitokea nchini Malawi ambapo alifukuzwa na kupewa hifadhi ya kisiasa nchini Tanzania. Taifa la Malawi liligubikwa na ghasia kutokana na machafuko ya kisiasa baada ya uhuru. Mhango alipoingia Tanzania alikuwa mwandishi wa habari, hivyo alianza kufanya kazi katika gazeti la Tanganyika Standard Dar es Salaam. Waandishi wa habari nchini Malawi waliishi kama ndege, waliishi kwa kutangatanga na kukosa amani kutoka na kuwindwa na vikosi vya serikali.
Kwa mfano Francis Pallock Mhango mwandishi wa Lukuni Press iliyokuwa inamilikiwa na Kanisa Katoliki alikamatwa Desemba 1981 akiwa ofisini mwake Lilongwe. Wakati huu mataifa mengi barani Africa yalikuwa katika mvutano mkali sana wa vita baridi kati ya Umoja ya nchi za Kisovieti pamoja na mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.
Mataifa mengi ya Afrika, kwa uchache kama Ghana, DRC, Sierra Leone (Upper Volta) viongozi wake waliuwawa wakiwa madarakani na wengine kupinduliwa kabisa. Hata Tanzania vuguvugu hili la kutaka kumng’oa Mwalimu kwa nguvu lilikuwepo. 1982 wakati hali ya siasa imeshatengemaa nchini Malawi, Reginald Mhango alitaka kurejea Malawi, siku moja kabla ya kuondoka alipenyezewa habari ya kuwa kuna mapinduzi yanataka kufanyika, na mapinduzi hayo yatahusisha kifo ambapo ilipangwa Mwalimu Nyerere apigwe risasi wakati wa misa katika kanisa Katoliki Oysterbay.
Reginald alikuwa muumini na mfuasi mkubwa wa sera na falsafa za Mwalimu Nyerere, habari hii ilimpa wahaka hata asijue cha kufanya. Wakati huu Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania alikuwa ni Hayati Dr. Augustine Mahiga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati wa Hayati Dr. Magufuli. Mtu aliyempenyezea taarifa Reginald Mhanga jina lake ni Abdallah Mhando, ambaye kwa hofu alimrai sana Reginald asitoe taarifa aliyompa kwa usalama kwani ingeweza kuwagharimu.
Reginald hakukubali, alivunja safari yake ya Malawi na kumchukua Abdallah Mhando na kumuunganisha na mtu mmoja aliyeitwa Charles Kizigha, Charles alikuwa mtu karibu sana na Mkurugenzi Idara ya Usalama Dr. Mahiga. Dr. Mahiga alisimamia vyema suala lile na Nyerere hakutokea tena Kanisani siku iliyopangwa kutekeleza tukio la mauwaji yake.
Waliopanga mapinduzi na mauwaji ya Mwalimu walikamatwa na kufikishwa Mahakamani na kusomewa mashtaka mbele Jaji Nassoro Mzava, na hatimaye walisiohusika waliachwa huru na waliokutwa na hatia waliswekwa gerezani. Hadithi hii inaelezwa kwa undani na Adarsh Nayar, aliyekuwa mpiga picha wa Mwalimu Nyerere, mtu aliyefanikiwa kupiga picha nyingi zaidi za Mwalimu Nyerere alipokuwa Madarakani, hata picha ya Mwalimu Nyerere inayotumika hivi leo maofisini, ni yeye ndiye aliipiga.
Reginal Mhango, alifariki 19 Februari 2010 nyumbani kwake Magomeni Mikumi Dar es Salaam. Alifanya kazi kama Mhariri Mkuu Daily News, The Guardian na magazeti mengine makubwa nchini, na amefanya kazi Malawi, Tanzania na Malawi katika nyakati tofauti.
Watu kama Reginald ni muhimu sana katika historia ya Taifa letu, huyu ni moja ya shujaa asiyetajwa. Katika wakati kama huu ambao tunaelekea kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Taifa letu, ni vyema tukataja watu kama hawa, pengine asifuata ushauri wa rafiki yake Abdallah Mhando aliyemrai asiongee, yamkini Mwalimu angeuawawa na hii ingebadili kabisa historia ya Taifa letu.