Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kenani Kihongosi amesema chama kinawaonya viongozi wanaosababisha usumbufu kwa madereva wa bajaji na pikipiki za kubeba abiria maarufu kama bodaboda na kusisitiza kuwa hakitawafumbia macho.
“Vijana wenzetu wa bajaji na bodaboda sio wahalifu, ni vijana wanaojitafutia riziki na ndiyo maana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliwasaidia na kupunguza faini zao kutoka Sh. 30,000 hadi Sh. 10,000,
“Hivyo, niwaombe wale wote wenye dhamana kuhakikisha wanawasaidia vijana hawa na sio kutoa matamko ambayo yanavunja mouo vijana wenzetu,
“UVCCM tutasimama imara kuwalinda vijana wenzetu kwani wajibu wetu ni kuwa sauti ya vijana wa Taifa hili,” alisema Kihongosi.
Kihongosi alitoa maagizo hayo alipohutubia maelfu ya vijana wakati wa kongamano la vijana kuhusu faida za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama na jumuiya zake, umuhimu wa sensa pamoja na uzinduzi wa nyumba ya Katibu wa UVCCM Mkoa wa Iringa.