Wizara ya Afya imetangaza vifo vya watu watatu vilivyosababishwa na ugonjwa ambao bado haujafahamika ambavyo vimetokea katika Kituo cha Afya Mbekenyera kilichopo Halmashauri ya Ruangwa mkoani Lindi
Kwa Mara ya kwanza taarifa za uwepo wa ugonjwa huo zilisikika Julai 12, 2022 mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzungumzia jambo hilo alipokuwa katika maadhimisho ya mkutano wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu la Kanisa Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Mganga Mkuu wa Serikali Dk Aifello Sichalwe katika taarifa yake iliyotolewa leo Julai 13 amesema Julai 5 na 7 mwaka huu Kituo cha Afya Mbekenyera kilipokea wagonjwa wawili wenye ugonjwa usio wa kawaida ambapo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi alitoa taarifa wizarani.
“Kumekuwepo na ugonjwa usio wa kawaida kutoka Kituo cha Afya Mbekenyera, ambapo Ndani ya siku tatu walipokea wagonjwa wawili katika kituo hicho wakiwa na dalili za homa, kuvuja damu (hususan puani), kichwa kuuma na mwili kuchoka sana,” amesema Sichalwe katika taarifa hiyo.
Hadi kufikia Julai 12 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 13, kati yao, watatu wamefariki dunia kwa mujibu wa Dk Sichalwe ambapo wagonjwa wawili waliokuwa wametengwa katika kituo hicho cha afya wamepona na kuruhusiwa kurudi majumbani mwao.
Wagonjwa wengine watano wamejitenga katika makazi yao ya muda kwenye kitongoji cha Naugo wilayani Kilwa huku watu waliotangamana nao wamekuwa wakifatiliwa afya zao kila siku na kwa mujibu wa taarifa hiyo hakuna aliyeonesha dalili za kufanana na wagonjwa.
“Mgonjwa mmoja ambaye amepona anaendelea na shughuli zake katia Kijijini Mbekenyera,” amesema Sichalwe.
Wataalamu wamebaini nini ?
Timu ya wataalamu kutoka idara ya Magonjwa ya dharura na Majanga, Epidemiolojia, Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Utafiti (NIMR), Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inaendelea kufanya uchunguzi kubaini ugonjwa huo.
“Sampuli za awali zilizopimwa katika maabara ya Taifa zimeonesha majibu hasi (negative) kwa ugonjwa wa Ebola, Marburg na Uviko-19. Tunaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa kiepidemiolojia na kitabibu pia tunasubiri matokeo ya vipimo zaidi vya maabara ya magonjwa ya Binadamu, Wanyama na Mkemia Mkuu wa Serikali,” amesema.
Aidha wizara imesema inaendelea kufanya jitihada nyingine ikiwemo kutafuta watu wengine wenye dalili za ugonjwa huo ili kutambua mapema na kuwatenga ili kuzuia ugonjwa usisambae.
Pia kuwatambua watu wote waliotangamana (Contacts) na wagonjwa wahisiwa/marehemu na kuwafuatilia kwa siku 21.
“Kutoa matibabu kwa wagonjwa waliobainika kuwa na dalili, kuwashauri wajitenge wakati wakisubiria majibu ya vipimo vya maabara, kutoa elimu kwa jamii kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari,” amesema Dk Sichalwe.
Hata hivyo, wananchi wameshauriwa kuwa watulivu wakati Wizara ya Afya ikiendelea kushughulikia suala hilo huku wakitakiwa kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya pale wanapojisikia kuumwa