Rais Samia Suluhu Hassan ametunukiwa shahada ya juu ya udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kutokana na mabadiliko makubwa ya maendeleo tangu alipoingia madarakani Machi 2021.
Rais Samia ametunukiwa udaktari huo jana Novemba 30, 2022 na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Jakaya Kikwete kwenye mahafali ya 52 ya Chuo hicho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Milmani City uliopo jijini Dar es Salaam.
“Kwa mamlaka niliyokabidhiwa, ninakutunuku digrii ya heshima ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hongera sana,” amesema Rais mstaafu Kikwete akimtunuku Rais Samia udaktari huo.
Akizungumza mara baada ya kutunikiwa shahada hiyo Rais Samia ameushukuru uongozi wa UDSM kwa kutambua na kuona mchango wake anaoufanya ndani ya nchi ya Tanzania huku akikiri kujaribu kuitafuta shahada hiyo lakini muda haukumpa nafasi.
“Suala la kupewa tuzo hii nimelipokea kwa unyenyekevu mkubwa, nilijiuliza maswali kadhaa sababu huko nyuma nilijaribu kuitafuta shahada hii lakini muda haukunipa nafasi,” amesema Rais Samia.
Miezi 11 iliyopita kiongozi hiyo mkuu wa nchi alisema alitamani kujiendeleza kimasomo lakini majukumu yalimzuia lakini tukio la leo limekamilisha ndoto yake ya kuwa daktari wa heshima
Maazimio ya senenti ya Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kikao chake cha 875 yalimpendekeza Rais Samia kutunukiwa shahada hiyo kutokana na mabadiliko makubwa yaliyoletwa na uongozi wake.
Kwa upande wa sekta ya uchumi baraza hilo limetambua juhudi zake katika kuimarisha kilimo na ufugaji, teknolojia, mawasiliano na nishati. Pia Upatikanaji wa fedha za msaada na mikopo nafuu iliyowezesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kutolewa huduma za kijamii ikiwemo maji.
Sambamba na hayo uamuzi wake wa kuboresha mpango wa sekta ya kilimo nchini wenye lengo la kutatua changamoto mbalimbali na kuongeza mazao ya chakula na biashara
Katika sekta ya utalii, jitihada za Rais Samia zimeonekena katikakuongeza watalii nchini kupitia filamu ya Royal Tour ambapo kufikia Juni 2022 ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 34 ya watalii.