Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguaji wa lango la handaki mchepuko litakaloruhusu maji yaanze kujaa katika bwawa la kuzalisha umeme la JUlius Nyerere.
Tukio hilo limepangwa kufanyika Desemba 22 likishuhudiwa na wageni 2,300 kati yao Watanzania 2,000 na ugeni wa watu 300 kutoka serikali ya Misri wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo.
Waziri wa Nishati, January Makamba alisema mpaka sasa ujenzi wa bwawa umefikia asilimia 78.68 ambayo ni hatua ya awali ya kuanza kujaza maji na inategemewa kuchukua misimu miwili ya mvua.
“Wakati mradi unaanza kutekelezwa ili kujengwa handaki (tuta) katikati ya mto ni lazima maji yachepeushwe kwa nji nyingine, ili yaendelee mbele yakupe nafasi ya sehemu kavu kujenga handaki lenye gharama ya sh235 bilioni,” alisema Makamba.
Alisema hatua hiyo itajibu mijadala ya baadhi ya watu waliodhani mradi huo hautokamilika kwa muda uliopangwa, lakini pia hata uwezekano wa kujaza maji utawezekana kutokana na hali ya ukame inayoendelea.