Mahakama Kuu ya Diveshi ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imewatia hatiani watu sita, wakiwamo watatu wa familia moja na kuwahukumu kwenda jela miaka 50 kwa kosa la kula njama kutaka kupindua Serikali ya Tanzania.
Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki mbele ya Jaji Dkt. Yose Mlyambina kwenye Masijala Ndogo ya Songea.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Seif Chombo, Abdallah Chombo, Mohamed Kamala, Athumani Chombo, Omary Mbonani na Rashidi Ally.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Yose alisema washtakiwa wanatuhumiwa kati ya Januari Mosi 2014 na Julai 13,2020, kwenye maeneo tofauti wilayani Tunduma mkoani Ruvuma na maeneo mengine nchini, kwa pamoja walikula njama ya kufanya ugaidi.
Wanadaiwa kula njama kuanzisha vita ya kidini vijulikanavyo Jihada na kuwashawishi vijana kuongeza nguvu kuipindua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanzisha Taifa la Kiislamu kwa kutumia nguvu na machafuko.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kwenye Kijiji cha Lumbukule na maeneo mengine wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa viongozi wao wanaishi Ruvuma, Lindi, Mtwara na Pwani na kwamba viongozi wachache walikamatwa huku wengine wakifanikiwa kukimbilia Msumbiji.