Rais Samia awafuta kazi Mkuu wa Wilaya wa Mtwara na DED wake

HomeKitaifa

Rais Samia awafuta kazi Mkuu wa Wilaya wa Mtwara na DED wake

Rais Samia Suluhu Hassan amewafuta kazi Mkuu wa Wilaya wa Mtwara Vijijini, Hanafi Msabaha na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Tatu Issike kwa alichokieleza kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi na kusababisha kurudishwa kwa kadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ametangaza uamuzi huo alipokuwa akihutubia hafla ya kufunga mafunzo ya uongozi wa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa mkoani Pwani leo, Jumapili Agosti 27,2023.

“Mkuu wa Wilaya anahongwa, mradi anaacha kwenda unakotakiwa anapeleka usipotakiwa, kiasi kwamba wananchi wanafika kurudisha kadi za chama, sisi huku tuna haja kubwa mmetuacha fedha mmepeleka kule na kadi zenu hizo.

“Sina imani na Mkuu wa Wilaya anayesababisha kadi zirudishwe, Mtwara, Mkuu wa Wilaya yako sijui Hanafi (Msabaha) namtimua leo siwezi kustahimili kadi za chama zinarudishwa, nini Mkuu wa Wilaya yupo DED yupo yeye na DED wake,” amesema.

“Nini watu wana shida anaulizwa anasema unajua kule wengi wapinzani, so what si Watanzania wale? Kwani wao sio watu, tena wamejenga maana kigezo ilikuwa wajenge atakayefika mbali ndiyo mradi upelekwe kwake,” ameeleza.

Aidha, katika hotuba yake Rais Samia amewasisitizia viongozi kuwatumikia wananchi ipasavyo na kusikiliza kero zao kama inavyotakiwa huku akiwasihi kuhakikisha wanakuwa macho katika kulinda vijana wa Tanzania.

Pia amewataka viongozi kupanga mipango ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea duniani.

error: Content is protected !!