Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Watanzania kuweka mbele maslahi ya taifa na kukataa migawanyiko ya kisiasa au itikadi. Akiwahutubia wananchi katika kilele cha Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa, lililofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma, Rais Samia aliwataka Watanzania kuwa wamoja na kutanguliza umoja wa taifa juu ya maslahi binafsi.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa mshikamano wa kitaifa, Rais Samia alisema, “Niwatake Watanzania kutanguliza maslahi ya nchi kabla ya maslahi binafsi, tuwakatae wote wanaotaka kutugawa kwa sababu za kisiasa au tofauti za kiitikadi, Watanzania ni wamoja, Tanzania ni moja, sisi ni mtu mmoja.” Alieleza kuwa umoja na mshikamano ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa, na akawataka wananchi kuendelea kuheshimu na kudumisha maadili pamoja na utamaduni wa Kitanzania.
Aidha, Rais Samia aligusia umuhimu wa tamasha hilo la utamaduni, akihimiza kuwa tamasha lijalo linapaswa kuendeshwa kwa msukumo mkubwa zaidi na kushirikisha sekta binafsi kwa kiasi kikubwa. Alieleza kuwa tamasha kama hilo lina uwezo wa kukua na kuwa tukio kubwa linalotafutwa na mikoa mingi kuwa wenyeji wake, iwapo litapewa matangazo sahihi na maandalizi mazuri.
Rais Samia pia alikumbusha kuwa utamaduni wa taifa unahusisha vipengele vingi, kuanzia namna wananchi wanavyoishi hadi matumizi ya lugha ya Kiswahili, ambayo alitaja kuwa ni kiungo muhimu cha utamaduni wa Tanzania. Alibainisha kuwa Kiswahili si tu lugha inayounganisha taifa, bali pia ni nyenzo muhimu ya kufungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania. “Kwetu sisi hatuwezi kuongelea utamaduni wetu bila kugusia lugha yetu pendwa ya Kiswahili. Ndiyo lugha inayotuunganisha na kuwa na utamaduni mmoja na lugha hii imefungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania,” alisema.
Hotuba ya Rais Samia ilisisitiza umuhimu wa kuenzi na kutangaza tamaduni za Kitanzania, huku akitoa wito wa kuendeleza mshikamano wa kitaifa na kutumia fursa zinazotokana na utamaduni, ikiwemo lugha ya Kiswahili, ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa taifa.