Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameishukuru Taasisi ya Merck kwa ushirikiano wao katika masuala mbalimbali hasa katika sekta ya elimu na afya nchini.
Akizungumza katika Mkutano wa 11 wa Merck Foundation Africa Asia Luminary uliofanyika leo Oktoba 29, 2024 katika ukumbi wa Johari Rotana jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema Tanzania inajivunia kushirikiana na taasisi hiyo kwani ushirikiano huo umeleta maendeleo makubwa.
Rais Samia akieleza malengo makuu ya mkutano huo yakiwa ni afya bora, elimu bora na ushirikiano aliweka wazi kwamba ili kuweza kuyafikia malengo hayo, hatua za haraka zinahitajika.
“Kwa upande wetu, Tanzania, mengi yameelezwa na Waziri wangu wa Jinsia, Maendeleo, na Usawa wa Kizazi. Lakini tunaendelea kuchangia kwa maana mijadala hii muhimu.” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameeleza mafanikio yaliyopatikana ndani ya uongozi wake wa miaka mitatu kwenye sekta ya afya ikiwa ni jitihada moja wapo ya kuyafikia malengo ya mkutano huo.
“Kati ya mwaka 2021 na 2023, tuliongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa kuwekeza na kujenga hospitali zaidi ya 127 za wilaya na vituo vya afya 367 nchi nzima.
Kwa upande wa elimu, Rais Samia amesema shule za sekondari kwa ajili ya wasichana 24 zimejengwa nchini ikiwa ni lengo la kuhakikisha kila mkoa unajengwa shule hizo maalum.