Serikali yatangaza nafasi za ajira 3,633 za ualimu

HomeKitaifa

Serikali yatangaza nafasi za ajira 3,633 za ualimu

Serikali ya Tanzania imetangaza ajira 3,633 za walimu wa masomo mbalimbali ikiwemo ya Biashara, Ushonaji, Uashi, Umeme, Ufundi magari, Uchomeleaji na Utengenezaji Vyuma, Sanaa, Useremala, pamoja na Afya ya Wanyama.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Desemba 13, 2024 kwa niaba ya Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa imekaribisha maombi ya kazi kutoka kwa Watanzania wenye sifa na uwezo wa kujaza nafasi 3,633.

Hata hivyo, Kwa mujibu wa taarifa hiyo yenye Kumb.Na.JA.9/259/01/B/109 zaidi ya asilimia 94 ya nafasi zilizotangazwa ni za walimu wa masomo ya Biashara wakiwa na nafasi 3,425.

Aidha, vigezo na sifa za muombaji vimeainishwa katika kila nafasi ambapo si lazima muombaje awe amehitimu chuo ngazi ya stashahada au shahada katika kada ya ualimu pekee hususan katika masomo ya ufundi kama Ushonaji, Uashi, Umeme, Ufundi magari, Uchomeleaji na Utengenezaji Vyuma.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by Moest Moest (@wizara_elimutanzania)

Itakumbukwa, Novemba 23, mwaka huu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Adolph Mkenda alidokeza kuwa Serikali ipo mbioni kutoa kibali cha ajira 4,000 za walimu wa masomo ya biashara.

Hivi sasa kuna upungufu mkubwa wa vitabu pamoja na walimu wa masomo ya biashara jambo ambalo huenda imekuwa sababu ya wanafunzi kutofanya vizuri kwenye masomo hayo.

Huenda uamuzi huo wa Serikali kutoa ajira nyingi kwa walimu wa masomo ya biashara ukachochea kwa kiasi ufaulu wa masomo hayo muhimu katika kutengeneza wataalamu wa uchumi.

error: Content is protected !!