Serikali yalipa zaidi ya shilingi bilioni 47 kwa watumishi walioondolewa kwa kughushi vyeti

HomeKitaifa

Serikali yalipa zaidi ya shilingi bilioni 47 kwa watumishi walioondolewa kwa kughushi vyeti

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizoandikwa na Gazeti la Rada tarehe 14 Aprili 2025, kuhusu malipo ya watumishi walioondolewa kazini kwa kosa la kughushi vyeti.

Gazeti hilo lilidai kuwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa Sherehe za Mei Mosi 2022 hayatekelezeki. Hata hivyo, Ofisi hiyo imeeleza kuwa maelekezo ya Rais yalitekelezwa kwa ufanisi na uadilifu, ambapo watumishi waliokuwa wakichangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii—PSSSF na NSSF—wamelipwa michango yao kama ilivyoelekezwa.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, watumishi 15,288 wameshalipwa jumla ya shilingi 47,020,753,222.23 kupitia mifuko ya PSSSF na NSSF. Ofisi hiyo imeelezea masikitiko yake juu ya upotoshaji uliotolewa na gazeti hilo na kusisitiza kuwa Mwanasheria wake hakuhusishwa kutoa maoni kabla ya taarifa kuchapishwa.

Serikali inawahakikishia wananchi kuwa haki ya watumishi hao imetekelezwa kikamilifu kulingana na maelekezo ya Rais Samia, na inasisitiza umuhimu wa kufuata maadili ya uandishi wa habari kwa vyombo vya habari.

error: Content is protected !!