Tanzania imepiga hatua katika viwango vya kimataifa vya Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa kupanda kutoka nafasi ya 97 mwaka 2024 hadi nafasi ya 95 mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF) iliyotolewa jana, licha ya Tanzania kupanda kwa nafasi mbili, alama za ujumla zimepungua kidogo kutoka 54.80 mwaka 2024 hadi 53.68 mwaka huu.
Ripoti hiyo inayotolewa kila mwaka imeonesha kuwa kupanda kwa nafasi ya Tanzania kunahusishwa na hatua zilizochukuliwa na serikali pamoja na wadau wa sekta ya habari katika kuboresha mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari na kukuza uhuru wa vyombo vya habari.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na mapitio ya sheria zinazohusiana na habari, ikiwemo Sheria ya Huduma Za Habari ya mwaka 2016 ambapo maboresho yamelenga kuondoa vifungu kandamizi na kuweka mazingira wezeshi kwa wanahabari.
Aidha, hatua nyingine zilizosaidia kupanda ni pamoja na kuimarika kwa mawasiliano kati ya serikali na vyombo vya habari kupitia majukwaa ya majadiliano ya wazi kumesaidia kujenga uaminifu na kuongeza uwazi katika upatikanaji wa taarifa.