Rais wa Findland awashukuru Watanzania kwa ukarimu

HomeKitaifa

Rais wa Findland awashukuru Watanzania kwa ukarimu

Rais wa Finland, Alexander Stubb, ametoa shukrani zake za dhati kwa Watanzania kutokana na ukarimu waliouonyesha wakati wa ziara yake ya kitaifa ya siku tatu aliyoianza nchini Mei 14, 2025. Stubb alieleza kuwa upendo na ukarimu wa Watanzania umeimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Finland, huku nchi hizo zikiwa na lengo la kuongeza ushirikiano katika sekta mbalimbali.

Akizungumza baada ya kutembelea Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam, Rais Stubb alisisitiza umuhimu wa utunzaji wa historia, urithi, na malikale ambazo zinaonyesha asili, chimbuko, na vifaa vilivyotumika katika historia ya binadamu pamoja na hifadhi za rasilimali bahari.

“Asanteni sana Watanzania kwa ukarimu mzuri tulioupata katika ziara hii ya kitaifa. Nimefurahi pia kutembelea Makumbusho ya Taifa. Mke wangu alikuwa hapa jana (juzi) na alisema ni mahali pazuri sana, panayo mpangilio mzuri, na sasa najua chimbuko la binadamu, najua asili yangu ni wapi,” alisema Rais Stubb.

Ziara ya Rais Stubb ilijikita pia katika kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Finland na Tanzania. Aliongeza kuwa kupitia Makumbusho ya Taifa, nchi hizo mbili zitapata fursa ya kuendeleza ushirikiano katika maeneo yenye fursa za kiuchumi na kijamii.

Rais Stubb aliweka wazi kuwa Tanzania na Finland zina uhusiano wa muda mrefu, na ziara hii itaimarisha zaidi ushirikiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.

error: Content is protected !!