Rais Samia afafanua mwenendo wa deni la taifa kwa dakika saba

HomeKitaifa

Rais Samia afafanua mwenendo wa deni la taifa kwa dakika saba

Rais Samia Suluhu Hassan, ametumia dakika saba kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu mwenendo wa deni la taifa na hatua zinazochukuliwa na Serikali kulidhibiti na kuhakikisha linaendelea kuwa himilivu.

Akihutubia Bunge, Rais Samia amesema kuwa ongezeko la deni la taifa limesababishwa na mchanganyiko wa mikopo iliyosainiwa katika awamu zilizopita lakini fedha zake kupokelewa katika awamu ya sita, pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.

“Ni vyema wananchi wakaelewa kuwa baadhi ya mikopo tuliyopokea sasa ilisainiwa miaka ya nyuma. Pia, mabadiliko ya thamani ya fedha yamechangia kuonekana kuwa deni limeongezeka kwa takribani trilioni 3.9,” alisema Rais Samia.

Rais alifafanua kuwa hadi Mei 2025, deni la taifa lilikuwa limefikia Shi trilioni 107.7, na kwamba Serikali inalipa kwa wakati mikopo hiyo huku ikihakikisha haina athari kubwa kwa ustawi wa uchumi.

Kwa sasa, malipo ya deni hilo yameongezeka kutoka Sh trilioni 8.2 mwaka 2020/21 hadi makadirio ya trilioni 14.2 kwa mwaka wa fedha 2025/26, kutokana na kuiva kwa mikopo ya muda mrefu, mabadiliko ya riba kimataifa, na kulipia dhamana kwa wawekezaji wa ndani.

Rais Samia pia alieleza kuwa Serikali imeanza kuhusisha baadhi ya madeni ambayo hayakutambuliwa awali kama sehemu ya deni la taifa, yakiwemo zaidi ya Sh trilioni 2.7 kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii kama PSSSF, NSSF na NHIF.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuongeza mapato ya ndani, kupunguza utegemezi wa mikopo, na kuhakikisha fedha zote za mikopo zinaelekezwa kwenye miradi yenye tija kwa taifa, huku maafisa masuuli wakitakiwa kuzingatia sheria na taratibu katika usimamizi wa mikataba.

error: Content is protected !!