Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonesha dhamira thabiti ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini kwa kufanya mageuzi makubwa ya kisera na kifedha. Moja ya mafanikio makubwa yanayoonekana ni ongezeko la bajeti ya Wizara ya Kilimo katika kipindi cha miaka mitano.
Katika mwaka wa fedha 2020/2021, bajeti ya Wizara ya Kilimo ilikuwa Shilingi bilioni 294.16. Hata hivyo, kufikia mwaka wa fedha 2025/2026, bajeti hiyo imepanda hadi kufikia Shilingi trilioni 1.24. Hili ni ongezeko la zaidi ya mara 4.4, linalodhihirisha wazi kuwa Serikali imeipa sekta ya kilimo kipaumbele cha juu.
Ongezeko hili la bajeti linaashiria juhudi za makusudi za Serikali katika kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kwenye Pato la Taifa, kuimarisha usalama wa chakula, na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, ambapo takribani asilimia 65 ya wananchi wanategemea kilimo kama chanzo kikuu cha kipato na maisha.
Kupitia uwekezaji huu mkubwa, matarajio ni kuwa sekta ya kilimo itaendelea kukua kwa kasi na kuchangia zaidi katika maendeleo ya uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi.