Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuongoza tena nchi kwa kipindi kingine, ambapo leo akiwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mbalizi, Mkoa wa Mbeya, ametoa ahadi kadhaa zenye lengo la kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Samia amegusia maeneo muhimu ya huduma za kijamii, miundombinu, kilimo na ustawi wa miji. Miongoni mwa ahadi alizotoa ni pamoja na:
Sekta ya Huduma za Jamii
- Elimu, afya, maji na umeme: Ameahidi kuendeleza jitihada za serikali katika kuboresha huduma hizi msingi kwa wananchi, kwa kuhakikisha zinapatikana kwa ubora na kwa karibu zaidi na wananchi.
Sekta ya Miundombinu
- Ujenzi wa barabara: Amethibitisha dhamira ya serikali yake kuendelea kujenga na kukamilisha barabara zote zilizoainishwa kwenye Ilani ya CCM kwa kasi kubwa na viwango vya kisasa.
- Ujenzi wa madaraja: Ameahidi kujenga madaraja makubwa na madogo ili kurahisisha usafiri na kuunganisha maeneo mbalimbali, hasa vijijini.
- Miradi maalum ya barabara: Ametaja miradi mahususi ya ujenzi wa barabara ikiwemo:
- Barabara ya Mbalizi – Shigamba
- Barabara ya Mbalizi – Mkwajuni Songwe
- Barabara ya Isonye – Kikonde

Wananchi wa Mbeya Mjini wakiwa kwenye Mkutano wa Kampeni za Mgombea Urais CCM, Ndg. Samia Suluhu Hassan
Sekta ya Kilimo
- Ruzuku kwa wakulima: Amewahimiza wakulima kuendelea kujisajili ili waweze kunufaika na mpango wa ruzuku unaotolewa na serikali.
- Mbolea na pembejeo: Ameahidi kuongeza kasi ya usambazaji wa mbolea ya ruzuku pamoja na pembejeo bora ili kuongeza tija katika kilimo.
Uendelezaji wa Sekta ya Mifugo
- Mradi wa machinjio ya Kitengule: Ameahidi kukamilisha ujenzi wa machinjio hayo ya kisasa ambayo yataongeza thamani ya mazao ya mifugo na kusaidia kukuza uchumi wa wafugaji na wakazi wa maeneo hayo.
Uboreshaji wa Hadhi ya Miji
- Mji wa Mbalizi: Mheshimiwa Samia ameahidi kulifanyia kazi ombi la wananchi wa Mbalizi la kutaka mji huo kupandishwa hadhi, ili kuendana na kasi ya maendeleo na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Samia Suluhu ameonesha kuwa anaendelea kusikiliza sauti za wananchi na kuzielewa changamoto zao, huku akiahidi kuyapatia majibu ya haraka kupitia mipango inayotekelezeka. Alisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa chama kinachojali wananchi na kutekeleza kwa vitendo yale yote inayoyaahidi.