Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limechukua hatua za dharura kukabiliana na changamoto ya upungufu wa umeme katika mikoa ya Mtwara na Lindi, kufuatia hitilafu ya kiufundi kwenye mashine ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia ya megawati 20 katika Kituo cha Hiari, Mtwara.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Bi. Irene Gowelle, Septemba 20, 2025 amewamba radhi wateja wa mikoa hiyo kwa usumbufu uliosababishwa na hitilafu hiyo.
“Tunatambua usumbufu unaowapata wateja wetu na tunaomba radhi kwa changamoto hii ya muda. Huduma ya umeme ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo tumechukua hatua za haraka kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika unaimarishwa,” alisema Bi. Gowelle.
Aliongeza kuwa TANESCO inapaleka mashine mpya ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia yenye uwezo wa megawati 20, hatua ambayo itaimarisha uzalishaji umeme na kukabiliana na upungufu wa umeme mara mashine hiyo itakapofungwa na kuanza kuzalisha umeme.
“Mashine hii mpya ipo njiani kuelekea Mtwara na mara itakapoanza kazi, tunatarajia kurejesha huduma kwa kiwango cha kawaida. Tunaomba wateja wetu waendelee kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha mpito,” aliongeza.
Pia ameeleza kuwa Shirika litaendelea kuwasiliana na wateja wa Mtwara na Lindi ili kuwajulisha hatua kwa hatua kuhusu jitihada za kurejesha huduma ya umeme katika hali ya kawaida.
Kwa upande wake, Meneja wa Vituo vya Uzalishaji Umeme kwa Gesi Asilia vya Mtwara I na II, Mhandisi Ludovick Maro, alisema mashine ya megawati 20 iliyopata hitilafu imesababisha kupungua kwa uzalishaji wa umeme, na kwa sasa mikoa ya Mtwara na Lindi inategemea zaidi Kituo cha Mtwara I chenye uwezo wa megawati 30.