Rais Samia Suluhu Hassan amesema nafasi alizowapa mawaziri na naibu mawaziri sio fahari, bali ni dhamana za kuwatumikia wananchi.
Amesema watakaoubeba uwaziri kama fahari wajipange kubadilishwa, akisisitiza hataona aibu kuwabadilisha kama ilivyokuwa awali, hadi pale atakapopata wale wanaofanya kazi kuendana na dhamira yake.
Sambamba na hilo, amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kufanya kazi kwa kuzingatia kauli mbiu ya Kazi na Utu, akisema utendaji wake ujikite kuujali utu wa Mtanzania.
Rais Samia ametoa kauli hiyo, Jumanne Novemba 18, 2025 alipozungumza katika hotuba yake baada ya kuwaapisha mawaziri na naibu mawaziri, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.


