Tanzania sasa ina umeme wa kutosha

HomeKitaifa

Tanzania sasa ina umeme wa kutosha

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Tanzania kwa sasa ina umeme wa kutosha na hivyo ukamilifu wa Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere umeondoa kabisa mgao wa umeme nchini.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo Novemba 26, 2025 wakati wa ziara yake katika Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) iliyoleng kujionea namna mradi huo unavyozalisha umeme na kujihakikishia kuwa uzalishaji unaendelea kwa ufanisi kama ilivyopangwa.

Waziri Ndejembi amesema kuwa tayari mradi wa Julius Nyerere umekamilika na una uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, kiwango ambacho kimeleta uthabiti wa upatikanaji wa nishati na kupunguza changamoto za upatikanaji umeme zilizokuwa zikijitokeza katika baadhi ya maeneo nchini.

“Tangu uzalishaji ulipoanza hapa, kumekuwa na maboresho makubwa katika usambazaji wa umeme na sasa Serikali inajikita kwenye ujenzi wa njia za kusambaza umeme ili kuufikisha katika maeneo mengi zaidi nchini”. Amesisitiza Mhe. Ndejembi

Amefafanua kuwa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika kuhakikisha mradi umekamilika kwa wakati na una uwezo wa kutoa umeme katika eneo la mradi na kuwafikia Watanzania.

Kuhusu ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa ujenzi unaendelea, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuhakikisha umeme wa uhakika unafika katika mikoa ya Kati, Kaskazini na Kanda ya Ziwa.

Aidha, amesema Serikali ipo katika hatua za kuanza ujenzi wa njia nyingine muhimu ya kusafirisha umeme kutoka eneo la mradi wa JNHPP hadi Mkuranga, ambayo itapeleka umeme katika Kongani ya Viwanda Mkuranga ambao pia utalisha Jiji la Dar es Salaam.

error: Content is protected !!