Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Bima ya Afya kwa Wote, inatarajiwa kuzinduliwa Januari mwakani.
Aidha, Dk. Mwigulu, amezitaka hospitali zote nchini zijiandae na bima ya afya kwa wote wakiwemo watoto, wanawake hususan wajawazito na wazee.
Alitoa maagizo hayo jana, alipozungumza na wananchi baada ya kukagua uharibifu wa miundombinu mbalimbali, ukiwemo mzani wa magari (Mpemba), Mahakama ya Mwanzo Tunduma na Soko la Machinga, katika ziara ya kikazi mkoani Songwe.
Dk. Mwigulu alisema hatua hiyo ni sehemu ya ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan, alizodhamiria kutekeleza katika kipindi cha siku 100 akiwa madarakani.
Alisema ahadi hizo, zinapaswa kuanza mara moja kama utoaji wa ajira za wahudumu wa afya 5,000, wauguzi na wakunga.
Alisema usaili wa wataalamu hao wa afya, ulianza Desemba 10, mwaka huu na unatarajiwa kukamilika wiki hii katika kila mkoa, ifikapo Januari mwakani, wataalamu hao watakauwa tayari katika majukumu yao.


