Manunuzi na bidhaa migodini yafikia trilioni 5

HomeKitaifa

Manunuzi na bidhaa migodini yafikia trilioni 5

Serikali imetangaza kuongezeka kwa manunuzi ya huduma na bidhaa kwa kampuni za kitanzania kwenye migodi inayomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 na kufikia shilingi trilioni 4.41 sawa na asilimia 88 ya lengo la shilingi trilioni 5 katika makusanyo ya mwaka 2024.

Akitoa takwimu za utoaji wa huduma na bidhaa za migodini, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mbali ya ongezeko hilo la mapato pia ajira zimeongezeka na kufikia ajira 18,853 kati ya ajira 19,356 zilizopo migodini sawa na asilimia 97 kufikia Disemba 2024.

“Manunuzi ya huduma na bidhaa za jumla ya kiasi cha shilingi trilioni 1.85 kati ya manunuzi ya shilingi trilioni 3.01 yalifanyika mwaka 2018 na sasa yameongezeka hadi kufikia Shilingi trilioni 4.41 sawa na asilimia 88 kati ya shilingi trilioni 5 ya manunuzi yote yaliyofanyika mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 26 ya mapato,” ameongeza Mavunde.

Mbali na mafanikio hayo Mavunde amesema kuwa Tanzania imeanza kupata mafanikio ya mpango wa serikali wa kuhakikisha kampuni za uchimbaji madini zinarithisha ujuzi kwa wazawa hususani kwenye nafasi nyeti ambazo Watanzania wanajifunza kutoka kwa wataalamu wa kigeni.

“Tayari mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Twiga Minerals Corporation (Barrick Gold) nafasi zote za juu za uongozi zinashikiliwa na Watanzania kwa asilimia 100 kupitia utaratibu wa kisheria wa urithishwaji wa maarifa na ujuzi” Amefafanua Waziri Mavunde

Novemba mwaka jana Tume ya Madini nchini ilitangaza orodha ya bidhaa na huduma zinazotakiwa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa na kampuni za kitanzania kwa asilimia 100 huku mafanikio ya hatua hiyo yakitarajiwa kutangazwa kwa mara ya kwanza na tume hiyo kupitia kanuni ya 13A.

Nayo sekta binafsi imehimizwa kuchangamkia fursa ya usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma migodini ili kuhakikisha fedha kiasi kikubwa inabaki nchini Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

error: Content is protected !!