Bandari ya Mtwara imeendelea kuhudumia meli za aina mbalimbali ambapo tarehe 18.01.2026 imepokea meli ya mizigo ya MV ANTHIA iliyobeba shehena ya magari pamoja na mitambo ya ujenzi kutoka nchini China.
Meli hiyo imeshusha jumla ya mizigo 323 yenye uzito wa tani 2,448.91. Mizigo hiyo imewasili kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kwa wateja mbalimbali waliopo Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Malawi na Burundi.
Akizungumzia kuhusu ujio wa meli hiyo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Kapteni Paul Mchwampaka amesema kuwa, hatua hiyo inaendelea kufungua milango ya kibiashara kwa Bandari ya Mtwara pamoja na kuchochea nafasi ya Bandari katika kuvutia Nchi jirani kupitishia shehena zake.
Kwa upande wa Wakala wa Kampuni ya Seafront Shipping Service Limited iliyoleta meli hiyo Bw. Erick Anthony ameonesha kuridhishwa na huduma zinazotolewa katika Bandari ya Mtwara. Wakala huyo amesisitiza dhamira ya kuendelea kuleta meli nyingi zaidi za aina hiyo katika Bandari ya Mtwara akieleza kuvutiwa na ufanisi mkubwa, weledi wa watendaji na ubora wa vitendea kazi vilivyopo Bandarini hapo.



