Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema kwa miaka mitano iliyopita kiwango cha mashirika ya umma yasiyo ya kibiashara kutegemea ruzuku ya serikali kimepungua kwa asilimia 12.8.
Mchechu amesema baadhi ya mashirika yaliyokuwa na changamoto za kifedha na kutegemea ruzuku ya serikali yameanza kujiendesha kwa faida.
Alisema hayo katika hafla ya taasisi na kampuni za umma kuikabidhi serikali gawio la Ikulu Dar es Salaam jana.
Kwa mujibu wa Mchechi mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mageuzi ya kiutendaji, kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani, na usimamizi madhubuti wa matumizi.
Alitaja taasisi zilizopiga hatua kubwa katika eneo hili ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Bodi ya Sukari Tanzania (TSB), BOdi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) na Wakala wa Vipimo (WMA).
Mchechu alisema hatua hizi zinaendelea kupunguza mzigo kwa serikali na kuelekeza rasilimali zaidi katika maeneo mengine ya maendeleo ya Taifa.


