Tanzania yapiga hatua matibabu ya saratani, yalenga kuwa kitovu cha tiba Afrika

HomeKitaifa

Tanzania yapiga hatua matibabu ya saratani, yalenga kuwa kitovu cha tiba Afrika

Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania inalenga kuwa kitovu cha utaalamu na mafunzo ya tiba ya saratani kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akihutubia Jukwaa la Kisayansi la IAEA mjini Vienna, Austria, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kinga, uchunguzi na matibabu ya saratani kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni ongezeko la chanjo ya HPV kwa wasichana wenye miaka 9 hadi 14 kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 98 mwaka 2026, huku vituo vya tiba ya saratani kwa mionzi vikiongezeka kutoka vitatu mwaka 2020 hadi sita mwaka 2026.

Pia serikali imeongeza teknolojia za kisasa za uchunguzi na matibabu, ikiwemo PET-Scan, MRI, LINAC, CT Scan na mammography, na inalenga kuwa na vituo tisa vya huduma jumuishi za saratani katika kanda sita za kimkakati Tanzania Bara na Zanzibar ifikapo 2030.

Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa IAEA na washirika wa kimataifa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kupitia mpango wa Rays of Hope, pamoja na kuiteua Taasisi ya Saratani Ocean Road kuwa kituo cha umahiri cha saratani kwa ajili ya mafunzo na kujenga uwezo wa wataalamu wa Afrika.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha huduma, utaalamu na teknolojia za kisasa za tiba ya saratani katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

 

error: Content is protected !!