Mkuu wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Jafar Haniu, ametoa siku tano kwa wananchi wa Kijiji cha Suma na wote wanaoishi pembezoni mwa Barabara ya Katumba–Mbambo–Tukuyu kuhama katika maeneo ya hifadhi ya barabara ili kuwezesha kuanza kwa kasi kwa shughuli za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Ametoa agizo hilo leo, Novemba 2, 2026, wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 79.4. Ziara hiyo imefanyika akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rungwe.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuondoa makazi na shughuli zao katika maeneo ya hifadhi ya barabara ndani ya siku tano, akionya kuwa watakaokaidi agizo hilo wataondolewa na Serikali na kutakiwa kurejesha gharama za zoezi hilo.
Aidha, ameitaka TANROADS Mkoa wa Mbeya kuongeza usimamizi kwa mkandarasi ili kuhakikisha kazi zinafanyika usiku na mchana na mradi unakamilika kwa wakati, akibainisha kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.


