Wavuvi katika mwambo wa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa, wamevua viboksi viwili ndani yake vikiwa na risasi 1,489 zinazotumiwa na bunduki aina ya SMG na nyingine za kivita.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijuakali amesema wavuvi hao kabla ya kufungua viboksi hivyo walidhani ndani yake kuna dhahabu. Alipopewa taarifa hiyo, yeye na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya walikwenda katika kijiji cha Kolongwe, na walipofika nyumbani kwa Mzee Jabile aliwakabidhi kiboksi kimoja alichokuwa nacho.
Kiboksi hiko baada ya kufunguliwa kilikuwa na risasi 739 tu, lakini kiboksi kingine kilichukuliwa na mvuvi mwingine ambaye alipotakiwa kukitoa ili kifunguliwe alikataa akidai apewe fedha kwanza akiamini kuwa ndani yake kuna dhahabu. Mzee Jabili alitafuta fedha alizodai mvuvi mwenzake akamkabidhi kijana ambaye aliziwasilisha na kukabidhiwa kiboksi kile.
Kiboksi cha pili baada ya kupatikana kilikutwa na risasi 750 ndani hivyo kufanya risasi zifike 1,489. Lijuakali alisema baada baada ya kupata viboksi hivyo walilazimika kwenda hadi mwambao mwa Ziwa Tanganyika ambapo viboksi hivyo vilipatikana kuona kwamba wangeweza kupata viboksi vingine, lakini hawakupata.
Vyombo vya Ulinzi na Usalama vinaendelea kuchunguza suala hilo, na wananchi wa Wilaya ya Nkasi wameombwa kutoa ushirikiano vya vyombo vya ulinzi na usalama.