Mkutano wa 76 wa Umoja wa Mataifa utaanza rasmi Jumanne Septemba 21, 2021 jijini New York (Makao Mkuu wa Umoja wa Mataifa), Marekani. Mkutano huo utakutanisha nchi wanachama 193 kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa, chombo kinachotunga sera za dunia na kujadili matatizo makubwa yanayoikumba dunia kwa ujumla na yale yanayokumba nchi moja kama mafuriko au magonjwa.
Kitarajiwe nini ndani ya wiki hii?
Mkutano huo unafanyika kwa siku 9 ambapo kutakiwa na vikao na hotuba kutoka kwa mataifa wanachama na mashirika makubwa na vikao vya baraza hilo vinaanza Septemba 21.
Wiki moja kabla ya mdahalo wa baraza hilo, Rais mpya wa Baraza la Umoja wa Mataifa, Abdulla Shahid kutoka Maldives atachaguliwa rasmi na kuchukua nafasi ya Rais aliyetangulia Volkan Bozkir kutoka Uturuki.
Viongozi 83 watatoa hotuba zao mbele ya hadhara ya baraza hilo na 23 watatoa hotuba kwa njia video (idadi hiyo inajumuisha viongozi wa nchi/serikali na viongozi wa mashirika ya kimataifa).
Kabla ya mkutano kuanza, lazima baraza liteue wajumbe 9 (Credentials Committee) ambao hawa kazi yao ni kukagua uhalali wa nyaraka za wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali ili kuhakikisha wasio na vigezo hawaruhusiwa kushiriki.
Baraza litapitisha ajenda ya mwaka huu ikiwamo kupanga vikao vya mwaka, kupitisha wajumbe wa Baraza la Usalama Umoja wa Mataifa, wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu na kupitisha bajeti ya mwaka.
Pia, katika wiki ya kwanza kutakuwa na majadiliano makubwa kuhusu mapinduzi ya Afghanistan, Myanmar pamoja na baa la UVIKO-19. Mwaka uliopita, licha ya mlipuko wa UVIKO-19, Umoja wa Mataifa ulikuwa na vikao 103 na kupitisha maazimio 320.