Diwani wa kata ya Tinde wilayani Shinyanga mkoani Shinyanga, Jaffari Kanolo, amekanusha taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, kwamba yeye (Kanolo) na Afisa Mtendaji katika kata yake, Latifa Mwendapole wamekuwa wakifanya upotoshaji kuhusu chanjo ya Uviko – 19.
Akizungumza jana Oktoba 28,2021 wakati wa kikao cha kamati ya afya ya msingi kuhusu tathmini ya utoaji wa chanjo dhidi ya Uviko 19 mkoani Shinyanga, Bi Sophia Mjema alisema “Diwani wa kata ya Tinde na Afisa Mtendaji wa kata ya Tinde wanatukwamisha kwa kufanya upotoshaji kuhusu Chanjo dhidi ya Covid 19. Naagiza hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao na hii iwe fundisho kwa watu wengine, hatuwezi kuona watu wanapotosha tukawaacha hivi hivi”
Leo hii kupitia gazeti la Nipashe, Diwani Jaffari Kalolo amekanusha taarifa alizopewa Mkuu wa Mkoa Sophia Mjema, na kusema kwamba taarifa hizo zina lengo la kumhujumu kisiasa.
“Najua hujuma hizi zimetengenezwa dhidi yangu sababu ya kudai gari la wagonjwa mwaka mzima sasa katika Kituo chetu cha Afya hapa Tinde, ambapo wagonjwa wamekuwa wakipoteza maisha sababu ya ukosefu wa gari. Lakin suala la kuzuia wananchi wasipate chanjo siyo kweli, sababu pia kupata chanjo ni hiari ya mtu, sasa mimi nitazuiaje?” amesema Kanolo.
Kanolo amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa jambo hili ili kuthibitisha anachokisema.