Kutokana na zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (Machinga) katika maeneo yasiyo rasmi na kuwapeleka katika maeneo waliyopangiwa, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetoa mapendekezo yake kwa Serikali juu ya namna bora ya kushughulikia suala hilo.
Mapendekezo hayo yametolewa kupitia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyosomwa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sillo Baran.
Sillo Baran ambaye pia ni Mbunge wa Babati Vijijini, amesema Kamati yake inakubaliana na mpango wa kuwaondoa machinga katika maeneo yasiyo rasmi lakini inaonya kwamba iwapo mapendekezo wanayotoa hayatafanyiwa kazi kutatokea mgogoro kati ya Serikali na wananchi.
Pendekezo la kwanza lilitolewa na Kamati hiyo ni kwamba Serikali kupitia mamlaka za Serikali za mitaa itenge maeneo rasmi kwa ajili ya machinga na maeneo hayo yawe yale yanayovutia ufanyaji biashara kwa kuwekewa miundombinu ya msingi na yawe karibu na maeneo yaliyozoeleka.
Pili, kamati imeshauri Serikali ihakikishe maandalizi ya maeneo rasmi ya biashara ya machinga pamoja na ujenzi wa miundombinu ya msingi yanafanyika katika mwaka huu wa fedha 2021/22 na kukamilika mwaka ujao wa fedha 2022/23.
Tatu, Kamati hiyo ya Bunge imesema ni lazima Serikali ifanye tathmini ya soko la ajira nchini ili kuja na mipango ya kuchochea ajira hasa kwa vijana.
Nne, Baran amesema ni lazima sasa suala la kurasimisha sekta isiyo rasmi liwe endelevu ili kuondokana na kuhamisha wafanyabiashara kila mwaka.