Maana ya utalii ni kutoka na kutembelea sehemu fulani aidha kwa kujifunza au kustarehe tu. Kila mtu ana aina ya vivutio anavyopenda kutembela, wapo wanaopenda wanyama, wapo wanaopenda tamaduni na mila, wapo wanaopenda utalii wa bahari na aina mbalimbali za utalii.
Kutalii hakukuhitaji kusafiri na kuenda mbali mara nyingine, kwani utalii wenye lengo la kujifunza unaweza kuanzia katika mazingira yanayokuzunguka kwanza. Kwa hapa Dar es Salaam hali ni tofauti kidogo, ni aghalabu kukuta wanyama kama vile ilivyo katika mikoa ya Arusha, Mara na Manyara. Dar es Salaam upo utalii hasa kuhusu mila na tamaduni za watu ambapo vyote hujumuisha ukoloni, dini, makabila, biashara ya utumwa na kadhalika.
Dar es Salaam yapo maeneo ambayo unaweza kutembelea yanayobeba historia na mafunzo makubwa sana, na uzuri wa maeneo haya haya kiingilio, unaweza ukachagua muda mzuri ukatembelea bila hata kutozwa kiwang chochote cha fedha. Na maeneo hayo ni kama yafuatayo.
1. Azania Front Lutheran Cathedral
Huwezi kutaja makanisa ya zamani Tanzania ukaliacha kanisa hili. Kanisa hili liko chini ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani Anglikan Tanzania. Jengo hili zuri limejengwa kati ya 1899 – 1902.
Kanisa hili zuri kabisa lipo barabara ya kivukoni mkabala kabisa na bahari ya Hindi ambapo ukiwa umeme kanisani upatapa taswira nzuri ya bahari na majengo marefu yaliyopo posta. Neno Azania limetokana la lugha ya kigiriki likiwa na maana ya Pwani ya Afrika Mashariki. Tafuta siku nzuri mwisho wa wiki, tembele eneo hili, ukifika utakuta mtu atayakutembeza bila kukudai chochote, isipokuwa tu atakuomba uchangie kanisa (sadaka) na hii ni hiyari yako, lakini eneo hili lenye utajiri wa historia halina kiingilio.
Baada ya vita ya kwanza ya Dunia Mjerumani aliposhindwa vita na koloni na Tanganyika na makoloni mengine ya Ujerumani kuchukuliwa na Uingereza, mali na hata makanisa ya Ujerumani vilichukuliwa na Uingereza. Kanisa hili kwa miaka takribani 30 liliwekwa chini ya Anglikan ya Uingereza, baadae likarudishwa na Lutheran ikiwemo mashule na hospitali.
2. Shule ya Msingi – Uhuru Mchanganyiko
Shule hii ipo mtaa wa Uhuru na Msimbazi Kariakoo. Shule hii ukipita kwa nje unaitazama unaweza kudhani ni shule ya kawaida sana, lakini inabeba historia kubwa ya Taifa letu. Shule hii amesoma Mwanaharakati Bibi Titi Mohammed na Mwanafasihi mkubwa wa fasihi ya kiswahili duniani Sheikh Shaaban Robert. Bibi Titi alisoma hapo 1934 hadi 1938. Shaaban Robert bado haijulikani alianza hapo muda gani, lakini ukifika hapo utaelekezwa na kupewa historia kubwa ya shule hiyo, ikiwemo watu wengi mashuhuri waliopita shule hiyo. Wakati akina Bi.Titi wanasoma hapo, shule hiyo iliitwa Kichwele.
3. Old Boma
Kati ya majengo yote ya kale yaliyojengwa na matumbawe, Old Boma ni jengo la kale zaidi kuliko majengo yote Dar es Salaam. Jengo hili lilijengwa na Mwana Sultan wa Zanzibar Majid bin Said mwaka 1866. Jengo hili lina hadhi ya tofati, malighafi zake kama milango, vitasa, madirisha na vya upekee na kuvutia sana.
4. Shule ya Pugu Sekondari
Jina la Mwalimu Nyerere limetokana na kazi yake ya kufundisha katika shule hii. Shule hii ukifika ina wingi wa historia ya watu ambao wameifanyia mengi sana nchi yetu. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifundisha hapo, Rais Benjamin Mkapa alisoma hapo, Spika aliyestaafu Pius Msekwa alisoma hapo, Prof. Ibrahim Lipumba, Prof. Kitila Mkumbo, Waziri Mkuu aiyepita Mizengo Pinda na wengine wengi tu. Ukifika hapo utaonesha walipokuwa wanalala, wanakaa kula chakula na vitu vingi vya zamani. Hakuna kiingilio.