Ziwa Victoria: Moyo wa Afrika

HomeMakala

Ziwa Victoria: Moyo wa Afrika

Ni ziwa ambalo limebahatika kuwa kwenye mstari wa ikweta na limezungukwa na nchi tatu za Afrika Mashariki: Tanzania, Kenya na Uganda pia ni moja ya maziwa makuu ya Afrika Mashariki na chanzo kikuu cha maji ya Mto Nile wenye urefu wa kilomita 6,650 na urefu unaufanya kuwa mto mrefu zaidi duniani ingawa vyanzo vingine vinakizana na taarifa hiyo.

Katika bara la Afrika, Mto Nile unakatiza katika nchi tano zikiwemo, Sudan, Uganda, Sudan ya Kusini, Ethiopia na Misri ambapo uacha neema kwenye sekta mbalimbali ikiwemo utalii, biashara, kilimo na usafirishaji.

Kabla ya kupewa jina la Ziwa Victoria na John Speke pamoja na Richard Burton baada ya kuamua kumtunuku malkia wa Uingereza Queen Victoria mwaka 1858, ziwa hili lilikuwa likijulikana kama Ziwa Nyanza huku historia ikisema kwamba Waarabu pia waliwahi kuvuka ziwani hapo mwaka 1160 na kufanikiwa kutengeneza ramani ya ziwa hilo.
Eneo

Ziwa Victoria ndiyo ziwa kubwa zaidi barani Afrika na lina ukubwa wa kilomita za mraba 68,800.Duniani, ni ziwa la pili kwa ukubwa likitanguliwa na Ziwa Superior lililopo Amerika ya kaskazini, kwa ukubwa huu nchi za Rwanda na Burundi zinaweza kuwa visiwa ndani ya ziwa hili.
Watumiaji.

Ziwa hili linahudumia wakazi takribani milioni 40 wa Afrika Mashariki na chakula ambacho ni samaki wa aina ya sato na sangara. Ziwa Victoria lina kina cha mita 84, ambao ni zaidi kidogo ya robo tatu ya uwanja wa mpira wa miguu.

Chanzo cha Ziwa Victoria

Asilimia 80 ya maji yote ya Ziwa Victoria yanatokana na mvua, asilimia 20 nyingine huchangiwa na mito inayomwaga maji yake ndani ya ziwa hilo, ukiwepo Mto Kagera. Masomo ya jiografia yanasema kwamba mara kadhaa Ziwa hili hukauka kabisa na mara ya mwisho kukauka ilikuwa miaka 17,000 iliyopita.

Na pia kama unakumbuka au kama ulikuwa umezaliwa mnamo Mei 21 mwaka 1996, kulitokea ajali ya meli ya MV Bukoba kuzama ziwani hapa na kupoteza maisha ya watu takribani 1,000. Ajali hii inasemekana kuwa ni moja ya majanga makubwa kuwahi kutokea kwenye usafiri wa majini katika ziwa hilo.

Utalii ziwani Victoria

Mwamba wa Bismarck au Jiwe la Bismarck, unaweza ukamwelezea mtu jinsi huu mwamba ulivyo na anaweza asiamini mpaka aone mwenyewe, lakini kwa kifupi ni mwamba huu umekaa mawe mengi yamepangwa juu ya mengine na upepo kidogo unaweza kuyaangusha mawe hayo kudumbukia ziwani lakini ndio lipo hivyo miaka yote.

Fukwe za Ziwa Victoria

Kama vile Dar Es Salaam au Zanzibar kulivyo na bahari na fukwe za kupumzika basi hata ziwani pia burudani haitofautiani sana. Mwanza kuna Tunza Resort, Bukoba kuna Bunena Stone Beach na Musoma kuna Palm Beach.

Ziwa Victoria lina visiwa zaidi ya 900 lakini ni visiwa 34 tu ambavyo vina makazi ya binadamu na vyote vinafikika kwa safari za boti kujionea tamaduni za jamii ziishio kwenye visiwa hivyo ikiwemo jamii ya Wakerewe.

Hifadhi za Taifa

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ambacho kipo magharibi kusini mwa ziwa hilo na kinajulikana kwa kuwa na sokwe, viboko na swala na uoto wa asili. Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane ambayo ina miaka saba tangu iwe hifadhi, inasifika kuwa na uoto wa asili na wanyama kama mamba, kobe, chui, swala, nyoka na nyani wa kipekee waitwao debraza wanapatikana katika hifadhi hiyo pekee nchini. Kufika katika visiwa hivi ni kwa kupitia Mwanza mjini kwa gari au ndege na kuelekea visiwani kwa boti. Je, umesikia mpango wa Serikali wa kulikutanisha Ziwa Victoria na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Vihatarishi vya Ziwa Victoria

Ziwa Victoria linakumbwa na matatizo ambayo yanaweza kuteketeza viumbe hai vyote vilivyopo majini humo, matatizo hayo yakiwemo:
1. Uchafuzi wa Mazingira.Utupaji taka ziwani toka kwenye miji iliyopo kando ya ziwa ikiwemo miji kama Bukoba, Mwanza na Musoma ya Tanzania; Kisumu, Kendu Bay na Homa Bay ya Kenya na Kampala, Entebbe na Jinja ya Uganda
2. Uoto wa magugu maji. Mimea inayokwamisha shughuli zingine kuendelea.
3. Uvuvi uliyokithiri kutokana ongezeko la uhitaji ya samaki hii pia inatokana na ongezeko la idadi ya watu waishio kwenye ukanda huo.

Utafiti wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Uasilia (IUCN) unaonesha kuwa asilimia 20 ya aina zote za viumbehai katika ziwa hilo waliozingatiwa kwenye utafiti huo wako katika hatari ya kuangamia.

Je, unahisi Ziwa Victoria linastahili jina la ‘Moyo wa Afrika Mashariki?

Kama unakubali, je, unafanya nini kuhakikisha ziwa hili linaendelea kuwa ‘Moyo wa Afrika Mashariki?’
Jibu ni rahisi, kwa kuanzia unaweza kusambaza makala hii kwa watu wako wa karibu ili kuhamasisha utumiaji bora wa ziwa hili kwa kutupa taka kwa utaratibu uliyowekwa na mamlaka na kufanya uvuvi kwa kuzingatia vizazi vijavyo

error: Content is protected !!