Baada ya kukiri kwamba alikuwa jambazi wa muda mrefu huku akiahidi kuwa raia mwema na kwamba kamwe hatafanya uhalifu, Jeshi la Polisi mkoani Geita limemsamehe Faida Komanya (34) aliyejisalimisha hivi karibuni na kukiri kwamba alikuwa muhalifu.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Henry Mwaibambe aliwaeleza waandishi wa habari na kusema kwamba mwananchi huyo alijisalimisha mwishoni mwa Novemba mwaka huu lakini licha yakujisalimisha na kusamehewa, baba yake mzazi aitwaye Komanya Bahebe anayeishi Kijiji cha Bugaragara , kata ya Ilolagulu wilayani Mbogwe amemkataa kumpokea.
“Alikiri kufanya matukio siku za nyuma ambayo ni matukio ya uporaji mikoa ya Geita, Shinyanga na Tabora na kwamba aliomba awe raia mwema baada ya kuona wenzake wengi wakiuawa,”
“Faida amewatajia baadhi ya matukio aliyoyafanya na askari wetu wa vikosi vya kupambana na wahalifu wakawa wameyakumbuka hayo matukio na hilo kundi lake, lakini tumeona haina haja ya kumfunga,” alisema Kamanda Mwaibambe.
Aidha, baada ya baba mzazi wa Faida kukataa kumpokea kwa kuhofia kuchomewa nyumba na wananchi, Jeshi la Polisi liliamua kumpeleka kwa mama yake kijiji cha Ifungadi, wilayani Nyang’wale ambapo alipokelewa vizuri na anaendelea kuishi hadi sasa.