Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema kuwa uongozi wa ACT Wazalendo umeiagiza ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa chama hicho kukusanya maoni ya wanachama kuhusu tume huru ya uchaguzi wanayoitaka. Amesema chama hiko kimeweka kipaumbele suala la tume huru ya uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na wa serikali za mitaa kwa mwaka 2024 unakua huru, haki na kuaminika.
“Kwenye kikao cha wadau wa siasa juu ya hali ya demokrasia nchini kilichofanyika Dodoma, suala la tume huru ya uchaguzi lilifanikiwa na pande zote. Kwetu sisi ACT-Wazalendo hatua inayofuata ni mjadala wa kitaifa kuhusu aina ya tume huru tunayoihitaji” alisema Shaibu
Shaibu pia alibainisha kuwa mbali na maoni ya wanachama, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa chama hicho iliagizwa kufanya rejea ya uzoefu wa mataifa mengine yenye tume huru za uchaguzi zilizopigiwa mfano pamoja na ripoti mbalimbali ikiwamo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba.