Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Muheza, Nassibu Mmbaga amesema bila uwepo wa mradi wa fedha za ustawi wa Taifa wa mapambano dhidi ya Uviko-19 ingewachukua miaka mingi kujenga vyumba vya madarasa 67 yakiwemo ya shule shikizi 10.
Mmbaga aliyasema hayo jana wilayani Muheza, mkoani Tanga wakati akielezea mafanikio ya fedha hizo katika kutatua changamoto kwenye halmashauri yake kupitia fedha mbalimbali zikiwemo za ustawi wa Taifa wa mapambano dhidi ya Uviko-19.
Alisema Muheza ilikuwa na upungufu wa madarasa 25 katika kipindi cha mwaka jana, hata hivyo utaratibu wa halmashauri hiyo wa kutenga Sh12.5 milioni za mapato ya ndani kila mwaka ili kukamilisha madarasa, mchakato unaokwenda sambamba na ushirikiano wa wananchi wa eneo husika.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia Sh1.4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 57 na shule shikizi 10. Ni fedha nyingi kwetu na ukipiga hesabu za haraka haya madarasa tungekamilisha kwa miaka 21 endapo tungejenga wenyewe.
“Tunatoa shukrani kwa Rais Samia maana hatujui tungefanya nini au jambo gani lingetokea ili kukamilisha madarasa 25 ambapo kila moja lina thamani ya Sh20 milioni, lakini tumepata zaidi madarasa zaidi ya mahitaji,” alisema Mmbaga.
Mkurugenzi huyo alisema hatua hiyo pia imepunguza mzigo kwa wananchi ambao kwa nyakati tofauti walilazimika kutoa michango kwa ajili ya ufanikishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa. Alisema wananchi wa Muheza walijiwekea utaratibu wa kushiriki ujenzi ikiwemo kuchimba misingi ili kufanikisha mchakato huo.
“Uwepo wa shule shikizi utasaidia kuwapunguzia umbali wa mwendo wanaotembelea watoto hasa wanaoanza shule ya awali hadi darasa la tatu.Watoto wamepata ahueni, pamoja na muda mzuri wa kukaa na kusoma kwa ufanisi,” alisema Mmbaga.
Mradi huo umekwenda kutatua kero ya uhaba wa shule katika maeneo ambayo hayakuwa na huduma hiyo, ikiwemo kata ya Tongwe ambapo wanafunzi walikuwa wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya 10 lakini sasa hivi wanatembea kilomita moja hadi mbili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Handeni, Maryam Ukwaju alisema walipokea Sh740 milioni za mradi zilitumika katika utekelezaji wa ujenzi vyumba vya madarasa 37, kati hivyo 22 vya sekondari 15 kwa ajili ya shule shikizi.
“Maeneo yote yaliyojengwa vyumba vya madarasa yalikuwa na uhitaji mkubwa kwa sababu watoto ni wengi. Baadhi yao walikuwa wanatembea muda mrefu hasa wanaoishi kata ya Bondo ambao walikuwa wanatembea hadi kilomita 30 kwenda na kurudi kufuata shule kuu ya Kwalua.
“Tusingepata fedha hizi, ingetuchukua muda mrefu kujenga vyumba hivi kwa sababu katika mwaka wa fedha, bajeti yetu ilikuwa ni kujengwa vyumba vitano. Ingetuchukua zaidi ya miaka mitano kukamilisha madarasa haya 37 ambayo ujio wa fedha za Uviko-19 umewezesha yakajengwa kwa miezi miwili,” alisema Maryam Ukwaju.
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule Chifu Mang’enya, Abdallah Khalid alisema uwepo wa vyumba vya madarasa hayo utaleta morali kwa wanafunzi wenzake wanaoanza kidato cha kwanza, akisema mazingira yamebadilika na ana imani watasoma kwa bidii.