ACT – Wazalendo yaahidi zahati moja kwa watu 1,000 ikipata ridhaa ya kuongoza nchi

HomeKitaifa

ACT – Wazalendo yaahidi zahati moja kwa watu 1,000 ikipata ridhaa ya kuongoza nchi

Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) kimesema kama kitapata ridhaa ya kuongoza nchi kitagharamia bajeti ya sekta ya afya kwa asilimia 100 kwa kuanzisha bima ya afya kwa wote inayotokana na mfuko wa hifadhi ya jamii.

Pia, kimesema kitadhibiti na kupambana na magonjwa sugu ya Ukimwi, kifua kikuu, ukoma, saratani, figo na kisukari kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya upimaji, chanjo na kutoa matibabu ya bure kuanzia ngazi ya zahanati na vituo vya afya. Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya 2025-2030 imeeleza kuwa itahakikisha taifa linakuwa na mfumo bora wa kimatibabu kwa watu wote unaozingatia usawa na ubora katika upatikanaji wa huduma ya afya.

Ilani hilo ilieleza kuwa Serikali ya ACT Wazalendo itafungamanisha mfumo wa bima ya afya na hifadhi ya jamii kwa wote utakaowezesha Watanzania milioni 18 kuwa wanachama wa mfuko wa hifadhi ya jamii na watu wote kupata matibabu bora. SOMA: Wajadili teknolojia matibabu mfumo wa chakula

Pia, ACT Wazalendo imeahidi kujenga zahanati mijini na vijijini ili kufikia lengo la kuwa na zahanati moja kwa watu 1,000 na kujenga hospitali kubwa tatu za kanda zenye hadhi, uwezo na viwango vya kimataifa katika mikoa ya Mara, Ruvuma na Singida.

Ilani hiyo imeeleza kuwa chama hicho kitaimarisha huduma za mama na mtoto kwa kuboresha miundombinu ya huduma ya mama na mtoto katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya na kusimamia upatikanaji wa huduma hizo bila malipo, wala michango yeyote ile.

Pia, chama hicho kimeahidi kuwa kikipata ridhaa ya wananchi kitapiga marufuku wajawazito kutakiwa kwenda kujifungua na vifaa vya kujifungulia. Sambamba na hilo ilani hiyo imesema ACT Wazalendo imeahidi kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria na kuangamiza mazalia ya mbu nchini kote kupitia Kampuni ya Kitaifa ya Tanzania Biotech Products Limited (TBPL).

Kuhusu afya ya akili, ilani ya ACT Wazalendo imeahidi kuweka mtaalamu wa afya ya akili kwa kila hospitali ya wilaya, kuanzisha programu za huduma za kisaikolojia na ushauri kwa njia ya mtandao na kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya.

 

error: Content is protected !!