Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limetangaza kuendesha safari maalum ya ndege kati ya Dar es Salaam na Dubai siku ya Jumapili, Machi 8, 2026, kwa lengo la kusaidia abiria walioathiriwa na kusitishwa kwa safari za kawaida katika ruti hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo leo Machi 6, 2026 safari hiyo maalum itahusisha ruti ya Dar es Salaam na Dubai, na inalenga kuwasaidia abiria waliokuwa na tiketi halali za safari zilizositishwa hivi karibuni.
Shirika hilo limeeleza kuwa safari hiyo si huduma ya kawaida ya kibiashara bali ni safari maalum ya kurejesha abiria (repatriation flight). Kipaumbele kitatolewa kwa abiria waliokuwa na tiketi za safari zilizokuwa zimepangwa kati ya Dar es Salaam na Dubai.
Air Tanzania imewataka abiria walioathirika kuwasiliana na ofisi zake ili kupata maelekezo na kuthibitisha safari zao kabla ya kuondoka.
Kwa maelezo zaidi, abiria wanaweza kuwasiliana na ofisi za shirika hilo kupitia namba +255 748 773 900 kwa Dar es Salaam na +971 54 464 5322 kwa Dubai.
Air Tanzania imetangaza safari hiyo maalum ikiwa ni siku chache tangu kusitisha safari za kawaida katika ruti ya Dar es Salaam na Dubai, Februari 28, 2026 kufuatia kufungwa kwa anga katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati kutokana na vita vinavyoendelea katika ukanda huo hatua iliyochukuliwa kwa kuzingatia usalama wa abiria, wahudumu wa ndege na ndege zenyewe.
Aidha, ATCL imewashukuru abiria kwa uvumilivu wao wakati wa kipindi hiki na kueleza kuwa taarifa zaidi zitatolewa kupitia njia rasmi za mawasiliano za shirika hilo.


