Bajeti ya maji yapaa kwa asilimia 61

HomeKitaifa

Bajeti ya maji yapaa kwa asilimia 61

Wizara ya Maji imeliomba Bunge liidhinishe Sh1.017 kama bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 ambayo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 kutoka Sh627.78 bilioni mwaka 2024/25.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni, Mei 8, 2025 Waziri wa Maji Juma Aweso amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya bajeti hiyo itatumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwa ajili ya ikiwemo kuongeza usambazaji wa huduma ya maji kwa Watanzania.

Aweso ameongeza kuwa kati ya bajeti hiyo zaidi ya Sh73.78 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo Sh55.70 bilioni ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa wizara, Ruwasa, Mfuko wa Maji na Chuo cha Maji na Sh18.08 bilioni zitaelekezwa kwenye matumizi mengineyo ya uendeshaji.

“Ninaomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya Sh1trilioni kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2025/26. Hii ni ongezeko dogo kutoka matumizi ya kawaida ya mwaka uliopita yaliyokuwa Sh 69.66 bilioni,” amesema Waziri Aweso.

Kwa upande wa miradi ya maendeleo, ambayo inachukua sehemu kubwa ya bajeti, Serikali imepanga kutumia Sh943.12 bilioni mwaka 2025/26, ikilinganishwa na Sh558.12 bilioni mwaka uliopita.

Waziri Aweso ameeleza kuwa bajeti hiyo imelenga kutekeleza miradi mikubwa ya maji vijijini na mijini, kuboresha vyanzo vya maji, kupanua huduma katika maeneo yenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji na kuimarisha taasisi za sekta hiyo kwa ajili ya kudumisha huduma endelevu.

 

error: Content is protected !!