Kwa mara ya kwanza katika historia, Bandari ya Mtwara inatarajiwa kuanza kupokea mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa gesi asilia katika eneo la Nanguruwe, Mkoa wa Mtwara.
Hatua hiyo imebainika baada ya ugeni wa wafanyabiashara na viongozi wa Kampuni ya ARA Petroleum Tanzania kufanya ziara maalumu katika Bandari ya Mtwara kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wa bandari hiyo kuhudumia shehena kubwa za mitambo ya mradi huo kuanzia Agosti, 2026.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Meneja wa ARA Petroleum Tanzania, Hilal Al Hinai, amesema lengo la ziara hiyo lilikuwa kutathmini miundombinu, vitendea kazi pamoja na ufanisi wa bandari katika kushughulikia mizigo mizito na mikubwa.
“Tumefanya ziara katika Bandari ya Mtwara ili kujiridhisha na uwezo wake wa kuhudumia shehena kubwa za mitambo ya uchimbaji wa gesi. Tumeridhishwa na miundombinu na maandalizi yaliyopo,” amesema Hilal.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mkuu wa Idara ya Masoko, Faraji Mbulalina, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wengi zaidi kutumia bandari hiyo, akieleza kuwa ina uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena mbalimbali kwa ufanisi.


