Bei elekezi vifurushi vya simu

HomeKitaifa

Bei elekezi vifurushi vya simu

Serikali imeagiza watoa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi wasibadili bei ya vifurushi vya simu hadi serikali itapotoa bei elekezi Januari mwakani.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha tathmini ya gharama za huduma za mawasiliano na inatarajia kushusha gharama za vifurushi.

Nape aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala kuhusu vifurushi vya simu ikiwamo intaneti na watumiaji wanahoji serikali inafanya nini kuhusu hilo.

Alisema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekuwa ikifanya tathmini kila baada ya miaka mitano na kwamba ya mwisho ilifanyika mwaka 2018 na gharama za huduma hizo zilikuwa kati ya Sh 2.03 na 9.35.

“Watumiaji wa huduma wengi wameeleza kuwa hawafurahishwi na huduma za mawasiliano zinazotolewa na hakuna mawasiliano mazuri kati ya watumiaji na watoa huduma hivyo kusababisha malalamiko juu ya huduma na hatua zinazochukuliwa na serikali,” alisema Nape.

Aliongeza, “TCRA inafanya tathmini kila baada miaka mitano na Desemba 2022 itakamilika, hivyo matokeo yatatolewa Januari…kwa hiyo nawaomba watoa huduma kutofanya mabadiliko yoyote ya bei za bundle katika kipindi hiki ambacho tathmini inaendelea hadi itakapokamilika.”

Nape alieleza kuwa katika tathmini hiyo, TCRA inaangalia uwekezaji uliofanywa na kampuni za simu na kodi wanayolipa ili kuwa na bei elekezi.

Aidha, ameongeza siku saba kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano waombe nafasi za ujumbe wa Bodi ya Baraza la Ushauri la Watumia Huduma za Mawasiliano (TCRA -CCC).

Nape alisema baraza hilo limekuwepo tangu TCRA ilipoanzishwa, lakini haijulikani hivyo wanalenga kuliimarisha ili liwasaidie kutengeneza uhusiano mzuri kati ya watoa huduma na watumiaji.

Alisema baraza hilo lina majukumu ya kuwakilisha maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano, kupokea na kusambaza taarifa za maoni ya wadau, kuwa na kamati ya watumiaji wa huduma ngazi za mikoa na kufanya mashauriano na wahusika katika sekta hiyo.

“Baraza lingekuwa na nguvu lingesimamia mahusiano yaliyopo kati ya watoa huduma na watumiaji lakini baraza hilo bodi yake imetetereka hivyo tumeongeza siku za maombi ili kupata wajumbe wa bodi,” alisema Nape.

Alisema jukumu la kwanza la bodi hiyo ni kukusanya maoni ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kuhusu utendaji, kanuni na sheria kisha wazipeleke wizarani kwa lengo la kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaboreshwa.

Nape alieleza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha linaondoa malalamiko na kutoelewana baina ya watumiaji wa huduma na watoa huduma za mawasiliano nchini.

error: Content is protected !!