Chama cha Wagumba Tanzania (CCWTZ) kimeahidi kusimamia haki za wagumba nchini ili waweze kuondokana na vitendo vya ukatili wanavyokumbana navyo ndani ya familia na jamii.
Pia kimeiomba serikali kuliangalia kundi hilo ambalo limesahaulika kwa kuzifanyia kazi changamoto wanazokumbana nazo ndani ya familia zao na jamii inayowazunguka.
Mwenyekiti wa chama hicho, Shamila Makwenjula alisema lengo la kuanzishwa kwa chama hicho ni kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na kundi hilo.
Alisema katika kusimamia haki ya kundi hilo kitawasaidia wanawake na wanaume wagumba kwa kutoa elimu kwa jamii ili waweze kuondokana na manyanyaso wanayokumbana nayo kwenye familia zao zinazowaathiri kisaikolojia.
Alisema wapo wagumba wanaotengwa na familia na kubaki wakiwa wameathirika kisaikolojia na kwamba hali hiyo si tu kwa kudni la wanawake pekee bali hata wanaume wenye changamoto hiyo.