Nikiwa nimekaa kwenye kibanda cha kupaka rangi kucha maeneo ya Mwenge-Mpakani alikuja msichana mmoja aliyekuwa ameloa chapachapa kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inaendelea muda huo.
Msichana yule alimuomba simu mpaka rangi na baada ya kupewa aliingiza namba na kuweka sikioni, alipiga simu bila mafanikio ghafla akaanza kusonya na kutukana huku akimtaja dalali, ndio ni dalali aliyempangisha chumba maeneo ya Mlalakuwa wiki kadhaa zilizopita lakini chumba hicho tayari kimeshashiba maji kiasi cha kuharibu vibaya mali za mwanadada huyo zilizokuwa chumbani humo.
Baada ya mimi kumaliza kupaka rangi nikaelekea stendi kupanda gari kuelekea nyumbani, nilikua mtu kama wa Sita hivi kuingia kwenye gari hilo lililokuwa likipitisha upepo mzuri lakini baada ya kutembea vituo viwili daladala hiyo lilijaa kiasi hewa kushindwa kuingia na waliosimama kukosa hata pakukanyaga.
Dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo hakuwa anajali hali ya abiria wake kwani yeye alikaa mbele akikenua huku akiita watu wengine wazidi kuingia kwenye daladala hilo.
Wapo watu kwenye maofisi, makampuni, shuleni na vyuoni na hata wanasiasa ambapo wanakuwa wanyenyekevu pindi waombapo wadhifa fulani na kutoa ahadi kadha wa kadha lakini baadae kukimba na wengine kuzima simu pale wapatapo nafasi hizo huku wengine wakiwa na tabia za dereva mwenye tamaa.
Bwana dalali pokea simu tumalizane kuhusu hiki chumba na dereva tafadhali tumejaa hebu tufikishe sisi kwanza.