Kuna mambo madogomdogo ambayo Wanaume wengi huwa hawayatilii maanani wakiamini sio wajibu wao kuyafahamu na kwamba ni mambo ya Wanawake pekee. Miongoni mwa mambo hayo ni tarehe za maadhimisho ya miaka ya mahusiano, rangi wapendazo wapenzi wao lakini kubwa tarehe za hedhi za mpenzi wake. Mwanaume unapaswa kutambua mzunguko wa hedhi ya mpenzi wako kwa kuwa ni muhimu na kujua huko kuna faida zifuatazo;
1. Kuepuka mimba zisizotarajiwa
Endapo Mwanaume utakua unajua mzunguko wa hedhi wa mpenzi wako basi mtaepuka mimba zisizotarajiwa kwani inakuwa rahisi kufahamu siku za hatari za mpenzi wako ambazo endapo ukijamiiana naye anaweza kupata ujauzito.
2. Ni sehemu ya kuonyesha mahaba
Kwa Wanawake, hakuna kitu kinagusa moyo wao kama wenzi wao kukumbuka vitu vidogovidogo kuhusu wao. Endapo unafuatilia mzunguko wa hedhi wa mpenzi wako basi hiyo ni sehemu ya wewe kuonesha kuwa unampenda kwa kumzawadia vifaa muhimu vya kujisitiri wakati wa hedhi zikiwemo taulo za kike.
3. Itakusaidia kumuelewa mpenzi wako
Mzunguko wa hedhi huambatana na mambo mengi kwa wanawake. Wapo ambao huumwa sana, wengine huwa na hasira zisizoeleweka na wengine hupenda kula. Endapo ukiwa unafahamu kinachoendelea kwa mpenzi wako, itakuwa rahisi kwako kumfariji pale anapokuwa kwenye maumivu, kumvumilia pale anapokuwa na hasira na kumnunulia chakula wala kutokumsema endapo atazidisha kiwango cha chakula chake cha kawaida.
Inashauriwa Mwanaume kuwa karibu na mpenzi wako pale anapokuwa katika siku zake za hedhi ili kumfariji, kumuonesha upendo na pia kuonesha kuwa upendo wako unaenda mbali zaidi ya kipindi akiwa sawa tu.