Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ametoa sababu ya kwanini daraja jipya la Tanzanite linatumika bure huku lile la Kigamboni watumiaji wanatozwa ushuru na kusema kuwa hii ni kutokana na masharti yaliyopo kwenye mikataba ya ujenzi wa madaraja hayo.
“Kama nilivyosema daraja la Tanzanite watanzania hawalipi na hawatolipa kwa sababu daraja lile limejengwa kwa asilimia mia moja pesa ya serikali, pesa ni ya mkopo masharti nafuu kutoka serikali ya Korea lakini mkopo ni pesa ya serikali, kwa sababu baada ya kukopa mwisho utalipa,”
“Kwa daraja la Kigamboni utaratibu uliotumika ni tofauti, pale serikali iliingia makubaliano na NSSF kwa ajili ya uwekezaji ule pale, na baada ya NSSF kuwekeza ile pesa lazima irudi na ndio tutakubaliana kwamba pale daraja lile watu watalipa tozo ndogo ili waweze kuchangia katika kurejesha fedha iliyotumika na NSSF,” alisema Mbarawa.
Mbarawa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 3, 2022 alipotembelea ujenzi wa daraja la Changombe jijini Dar es Salaam kufuatia kuwepo kwa maswali kwa nini daraja la Kigamboni wananchi wanalipishwa tofauti na Tanzanite.