Historia: Huu ndio upande wa Kariakoo usioujua

HomeMakala

Historia: Huu ndio upande wa Kariakoo usioujua

Labda nikuulize, ni picha gani hukujia kichwani mwako usikiapo neno kariakoo? Kwangu mimi ni msongamano wa watu lukuki, msururu wa biashara ndogo, kubwa na zile za kati. Kama hujajui maghorofa, basi utayajua kariakoo. Ni aghalabu kukuta Mtanzania na Wana Afrika mashariki walio wengi haijui Kariakoo, hata kama si kwa kuzuru eneo hilo, basi angalau kwa jina tu.

Imani yangu inanituma kukujuza jambo kuhusu eneo hili la kariakoo, najua wengi mna taswira ya maghorofo, msongamano na fujo za watu, ila mimi nataka kukurudisha nyuma zaidi kwenye karne ya 17 na 18, wakati ambao kariakoo ikivamiwa sana na Wafanyabiashara ya watumwa. Wakati leo hii tunapishana kwa uhuru tukiwa na bidhaa zetu vichwani na mikononi, miaka 400 iliyopita walipita watu hapa wakiwa na nyororo shingoni, kifua vyao vikiwa wazi na migongo yao ikitamalaki miale ya mijeledi, huo ni upande wa kariakoo usioujua.

Biashara ya utumwa kukoma, haina maana utumwa ulikoma, la hasha!! Mwanzoni mwa karne ya 19 eneo la kariakoo lilitwaliwa na mwana Sultani wa Zanzibar, Said Majjidi. Mwana huyo mwenye damu ya kifalme kutoka Oman, alilitwaa eneo la kariakoo la kulifanya Shamba binafsi kwa miaka dahari. Kwa visa na kadhia za mjerumani basi mwarabu akaona isiwe tabu, akaliuza shamba lake la hekta 200 kwa Mfanyabiashara wa kijerumani ambaye alikodishia vipande vidogo vya ardhi wazawa kwa shughuli mbalimbali kama kilimo na makazi.

Waingereza na mataifa mengine ya ulaya yalijitahidi kukomesha biashara ya watumwa. Watumwa waliotolewa mikoani na hata nje ya Tanzania, walipitia Dar es Salaam, Bagamoyo na Tanga kuelekea Zanzibar. Baada ya mkataba wa Zanzibar wa 1873 kusainiwa kusitisha biashara ya watumwa, bado watumwa waliuzwa kwa siri kwakuwa si kila Taifa au mfanyabiashara aliridhia kuacha biashara yenye faida kama hiyo. Watumwa waliachwa huru kutoka maeneo mbalimbali, wote walijazana Kariakoo. Eneo la Kariakoo wazungu hawakulipenda, liliachwa kwa ajili ya watu weusi.

Kariakoo leo hii sio eneo baguzi, halijui rangi kwakuwa watu wenye asili ya mataifa na mikoa mbalimbali wanashuhudia upendo eneo hili, ila wakati huo, kariakoo ilikuwa makazi rasmi ya watu weusi, naam, kulitengwa kwa minajili ya watu wote weusi, na huku wale wazungu wakivinjari kwenye makazi yao walipata pepo mwananana katika maeneo kama Oysterbay. Sensa ya 1913 inatwambia kuwa kati watu weusi 24,000 walioishi Dar basi 15,000 waliishi kariakoo.

Kufikia 1914 serikali ya Ujerumani ikalichukua eneo la kariakoo kutoka kwa mfanyabiashara yule, kwakuwa mfanyabiashara yule aliuza eneo lile kiholela, serikali ya ujerumani ilidhamiria kulijenga kwa ajili ya makazi ya watu weusi. Ni wakati huo ndio biashara zikaanza kupamba moto, hali ya uchumi ikaanza kuimarika eneo hili. Bahati mbaya vita ya kwanza ya dunia ikaibuka, ujenzi na uzinduzi wa eneo lile ukasuasua.

Muingereza alivamia eneo hilo na kulimiliki, akaligeuza kutoka eneo la biashara na makazi ya watu hadi kambi ya wanajeshi wabeba mizigo watembea kwa miguu, maarufu kama “Carrier Corps”.

Wakati Muingereza akilifanya eneo hili kama kambi, ndipo jina KARIAKOO likaanza kushika. Wakazi wa eneo hili walishindwa kabisa kutamka neno “Carrier Corps”, kila walipojaribu wakajikuta wakisema KARIAKOO, Basi ndio hadi leo Kariakoo.

Askari wale hawakuwa mahususi kwa ajili ya mapigano, bali waliandaliwa kwa ajili ya kubeba mizigo kama silaha na chakula wakati wa vita. Kambi za Carrier Corps zilikuwapo katika maeneo kama Mtwara, Dar es Salaam na Zanzibar. Na hawa walikufa sana kwa uchovu wa kutembea umbali mrefu, maradhi na kushambuliwa wakati wa vita kwani hawakuwa wanajeshi.

Moja kati ya alama inayoishi ya “Carrie Corps” ni sanamu ya askari pale posta maarufu maarufu kama ‘Askari Monument’ iliyowekwa mwaka 1927 na Uingereza baada ya vita ya kwanza ya dunia. Kwa makala hii fupi bila shaka una taswira mbili kichwani mwako kuhusu eneo la kariakoo, ukubwa wa biashara uliopo leo, umebebwa na mikasa mingi ya utumwa, ubaguzi, vita na kilimo. Hii ndio Kariakoo..

error: Content is protected !!