Hospitali ya Rufaa Manyara yaanza kutoa huduma za kusafisha figo

HomeKitaifa

Hospitali ya Rufaa Manyara yaanza kutoa huduma za kusafisha figo

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara imepiga hatua katika kuboresha huduma za afya za kibingwa kwa wananchi baada ya kuzindua rasmi huduma ya usafishaji damu (dialysis) na kipimo cha mfumo wa chakula (endoscopy).

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali ya awamu ya sita katika kuimarisha huduma za afya kwa ngazi ya mikoa na kupunguza gharama kwa wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika mikoa jirani.

“Huduma hii ni ya kisasa na muhimu sana kwa wakati huu, hasa ikizingatiwa kuwa magonjwa ya figo yanaongezeka kwa kasi duniani,” Amesema Sendiga.

Mradi huo mkubwa umegharimu kiasi cha Shilingi milioni 522.5, ambazo zilitumika kununua mashine sita za kusafisha damu, mashine ya kupima mfumo wa chakula, na kufanya ukarabati wa jengo litakalotumika kutoa huduma hizo.

Awali, wagonjwa waliokuwa wakihitaji huduma za kusafisha damu walilazimika kwenda Hospitali ya Rufaa ya Haydom au hospitali nyingine zilizoko mbali, jambo lililoongeza gharama na usumbufu mkubwa kwao na familia zao. Kwa sasa, huduma hiyo inapatikana mkoani Manyara, na hivyo kuondoa adha ya kusafiri umbali mrefu.

Aidha, kiasi cha Shilingi milioni 29.8 zilitumika kwa ajili ya mafunzo kwa watumishi wanaotoa huduma hizo maalum.

error: Content is protected !!